Mchungaji Mashimo awahimiza Watanzania kulinda amani atoa wito kwa viongozi wa dini





Na Mwandishi wetu

MCHUNGAJI wa Kanisa Christian Assembly,Daudi  Mashimo, amewapongeza Watanzania kwa kuendelea kulinda amani ya nchi, huku akitoa wito maalum kwa viongozi wa dini wa madhehebu yote kusimama pamoja na kuwa sauti ya faraja na umoja kuelekea Sikukuu ya Krismasi.

Mashimo ametoa wito huo Jijini Dar es salaam mapema leo Novemba 23,2025 wakati akizugumza na waandishi wa habari.

Amesema Katika  kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ya Christmas viongozi wa dini kutoka  madhehebu yote wanapaswa kuwa kitu kimoja ili kuhakikisha Taifa linapata faraja, amani na utulivu, badala ya kutumia maumivu ya wananchi kama nyenzo ya kuchochea migawanyiko

“Tunapokwenda kusherekea sikukuu, naomba viongozi wa dini tuwe pamoja, siyo kipindi cha Watanzania kutupiwa mizigo ya kuwaumiza,” amesema.

Mchungaji Mashimo amesema  hakuna Serikali yoyote duniani iliyokamilika, hivyo mshikamano wa kitaifa ni muhimu wakati wote.

Amesema kuwa Sikukuu ya Krismasi inapaswa kuwa chombo cha kuwaunganisha Watanzania ili wawe kitu kimoja na kujenga Taifa lenye upendo na uvumilivu.

“Nipo upande wa Mungu ambaye yupo katika dhamana ya nchi hii,” amesema, akiongeza kuwa maumivu yaliyopo yasigeuzwe fimbo ya kukumbushana matatizo, bali yawe msingi wa kujenga na kuimarisha Taifa.

Aidha amewatakia  Watanzania Krismasi njema, akisema ni maombi yake Yesu Kristo azaliwe upya katika mioyo ya watu wote.

Comments