BODI YA FILAMU TANZANIA NA BODI YA UTALIII TANZANIA ZAAZIMIA KUIMARISHA NA KUENDELEZA USHIRIKIANO
Na Mwandishi wetu
KATIBU Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Dkt. Gervas Kasiga amekutana na kikao na Mkurugenzi wa Idara ya Masoko ya Bodi ya Utalii Tanzania Ernest Mwamwaja aliyemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Ephraim Balozi Mafuru katika kikao hiki kilichofanyika leo Alhamis ya tarehe 8 Januari, 2026 katika ofisi za Bodi ya Utalii Tanzania, Jijini Dar Es Salaam.
Shabaha kuu ya kikao hiki ilikua namna bora ya ushiriki uliopo kati ya Bodi ya Filamu Tanzania na Bodi ya Utalii Tanzania katika kutafuta fursa za Utalii zilizopo nchini Tanzania kupitia filamu na michezo ya kuigiza.
Aidha, Dkt. Kasiga aliambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Filamu, Emmanuel Ndumukwa pamoja na viongozi wa Mradi wa Guardians of The Peak Ram Ally na Bi. Shuyan Wangu (Elizabeth Mrembo) ambao ni wadau wakubwa wa filamu na utalii nchini Tanzania.
Itakumbukwa kwamba mradi wa Guardians of the Peak unaoingia msimu wake wa pili sasa, unaandaa makala ya filamu inayolenga kuhamasisha shughuli za utalii katika Mlima Kilimanjaro, kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kuongeza uelewa wa mabadiliko ya tabia nchi katika jamii.
Hivyo, ushirikiano kati ya Bodi ya Filamu Tanzania, Bodi ya Utalii Tanzania na Mradi wa Guardians of the Peak ni fursa mpya ya kuutangaza utalii wa Mlima Kilimanjaro kupitia filamu ya nje ya nchi yetu ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutumia filamu kuutangaza utalii wetu.
Bodi ya Filamu Tanzania inaendelea kuchukua hatua za makusudi za kufungua fursa mbalimbali za kitasnia kupitia kwa wadau na muhimu katika sekta ya filamu na michezo ya kuigiza ili kutumia wigo wa fursa kwa ajili ya wanatasnia wote.
Endelea kurasa zetu za mitandao ya kijamii kupata habari na matukio muhimu kutoka Bodi ya Filamu Tanzania.




Comments
Post a Comment