ELAF YAIOMBA SERIKALI KUHESHIMU MAAMUZI YA MAHAKAMA
Na Mwandishi wetu
MKURUGENZI wa Kituo cha Msaada wa Kisheria cha Everlasting Legal Aid Foundation (ELAF), Wakili Khamisi Masoud, ameiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na watumishi wake kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia misingi ya Katiba na Sheria za nchi, sambamba na kuheshimu maamuzi ya mahakama.
Wakili Masoud ametoa kauli hiyo leo Januari 26, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia mgogoro wa ardhi kati ya Paulina Ndungule na Pili Kafuye ulioanza mwaka 2015, ambapo mahakama imeshatoa hukumu ikimtambua Paulina Ndungule kuwa mmiliki halali wa eneo hilo.
Alisema serikali ipo kwa ajili ya kusimamia sheria na haki, akisisitiza kuwa kiongozi au mtumishi yeyote anayekiuka au kudharau amri ya mahakama anahatarisha misingi ya utawala wa sheria na kuvunja uhalali wa kimaadili wa uongozi wake.
“Mahakama inapotoa uamuzi kwamba haki ni ya mtu fulani, basi madai na jinai ni mambo mawili tofauti. Katika mgogoro wa ardhi, mahakama tayari imeshathibitisha nani mmiliki halali wa eneo husika,” amesema Wakili Masoud.
Aliongeza kuwa tabia ya baadhi ya watu kujipa mamlaka ya kudharau maamuzi kuanzia ngazi za kimila hadi Mahakama Kuu ni jambo hatari kwa mustakabali wa taifa, akionya kuwa endapo hali hiyo itaachwa iendelee, wananchi wataanza kuikosa imani mahakama na kuamini nguvu za watu binafsi badala ya sheria.
Wakili huyo alisema kutoheshimiwa kwa maamuzi ya mahakama kunachochea migogoro, chuki na vurugu katika jamii, hali inayoweza kupelekea kujengeka kwa utawala wa mabavu badala ya utawala wa sheria, jambo linaloathiri amani na haki nchini.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Mirathi, Zawadi James, amesema mgogoro huo wa ardhi ulianza mwaka 2015 kati ya Paulina Ndungule na Pili Kafuye, ambapo marehemu Paulina Ndungule ndiye aliyefungua kesi katika Baraza la Ardhi la Kata na kushinda.
Zawadi amesema baada ya kushindwa katika baraza hilo, Pili Kafuye alikata rufaa kwenda Mahakama Kuu, lakini pia alishindwa, huku akidai kuwa wakati kesi ikiendelea, Pili Kafuye alianza kujenga kwenye eneo lenye mgogoro lenye ukubwa wa hekta tano na nusu, akijenga katika eneo la takribani hekta moja na nusu.
Aliongeza kuwa baada ya hukumu ya Mahakama Kuu, Pili Kafuye alikata rufaa kwenda Mahakama ya Rufaa ambayo ni mahakama ya mwisho nchini, ambapo mahakama hiyo pia ilitoa hukumu ikimtaka aondolewe katika eneo hilo na kulikabidhi kwa msimamizi wa mirathi.
Naye Sebastian Mathias, ambaye alikuwa shahidi katika mauziano ya kiwanja hicho, amesema muuzaji halali wa kiwanja hicho alikuwa mjomba wake anayefahamika kwa jina la Mpendakula, akisisitiza kuwa mauziano yalifanyika kwa kufuata taratibu halali.




Comments
Post a Comment