BODI YA FILAMU TANZANIA YACHANGIA GHARAMA ZA MATIBABU KWA WAGONJWA WA OCEAN ROAD

 




Na Mwandishi wetu

KUELEKEA maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Bodi ya Filamu Tanzania imetoa mchango wa kugharamia matibabu kwa baadhi ya wagonjwa wanaopatiwa huduma katika Taasisi ya Saratani Ocean Road iliyopo Dar es Salaam, leo tarehe 6 Machi 2026.

Mchango huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya kuonesha mshikamano wa kijamii na kuwafariji wagonjwa wanaopambana na ugonjwa wa saratani, hususan katika kipindi hiki kinachoelekea kuadhimisha nafasi ya wanawake katika jamii.

Ujumbe wa watumishi wa Bodi ya Filamu Tanzania uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dkt. Mona Mwakalinga na Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Bi. Asha Ngatila, ambapo walipokelewa na Bw. Malkiory Niniko, Meneja wa Huduma za Ustawi wa Jamii kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road.

Akizungumza wakati wa kupokea mchango huo,  Niniko aliishukuru Bodi ya Filamu Tanzania kwa moyo wao wa kujitoa na kujali jamii, akieleza kuwa mchango huo utasaidia kuwapa faraja na matumaini wagonjwa wanaoendelea na matibabu katika taasisi hiyo.





Naye Dkt. Mwakalinga alieleza kuwa Bodi ya Filamu Tanzania itaendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii zinazolenga kusaidia makundi yenye uhitaji na kuimarisha mshikamano ndani ya jamii.

@chuma_kaole @oceanroadcancerinstitute

Comments