MAKONDA AWATAKA VIONGOZI WA MICHEZO KUTEKELEZA AHADI ,AONYA WASIOTIMIZA KUNG'OLEWA
- Get link
- X
- Other Apps
Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema ofisi yake itaanza kufuatilia utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na viongozi wa mashirikisho ya michezo nchini na endapo itabainika kuwa hazijafikia hata asilimia 20 ya yale waliyoahidi wakati wa uchaguzi, wizara itashirikiana na wanachama kuleta mabadiliko ya uongozi.
Makonda ametoa kauli hiyo mapema leo Machi 13, 2026 katika mkutano wa viongozi hao na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) uliofanyika katika Benjamin Mkapa Stadium jijini Dar es Salaam.
Amesema viongozi wengi waliingia madarakani kwa kutoa ahadi nyingi kwa wanachama wao lakini utekelezaji wake umekuwa mdogo.
“Viongozi wa mashirikisho ya michezo nchini wanaoshindwa kutekeleza ahadi walizozitoa kwa wanachama wao wapo hatarini kung’olewa madarakani na mimi nitashirikiana na wanachama kuwaondoa,” amesema.
Makonda amesema serikali haitaridhika kuona viongozi wanaendelea kushikilia madaraka bila kuonesha matokeo katika maendeleo ya michezo nchini.
Ameeleza kuwa amepewa jukumu la kuhakikisha sekta ya michezo inaleta matokeo kwa taifa, hivyo viongozi wa mashirikisho wanapaswa kuwajibika kwa wanachama wao pamoja na maendeleo ya michezo kwa ujumla.
Aidha, amewataka viongozi hao kuimarisha uwazi katika uongozi wao na kujitathmini kuhusu utekelezaji wa ahadi walizotoa wakati wa kuomba kura kutoka kwa wanachama.
“Nyinyi mlipata nafasi hizi kwa kupigiwa kura na wanachama wenu. Ni lazima mujiulize mmetimiza kwa kiwango gani ahadi mlizotoa kwa waliowachagua,” amesema Makonda.
- Get link
- X
- Other Apps


Comments
Post a Comment