NONDO KUMPELEKA BABA LEVO MAHAKAMANI
Na Mwandishi wetu
MWENYEKITI wa Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo, Abdul Omary Nondo ametangaza kumfungulia kesi ya madai ya kashfa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini Clayton Revocatus Chipando maarufu "Baba Levo" akimtuhumu kusambaza taarifa za uongo zinazodai kuwa alijiteka mwenyewe katika matukio mawili tofauti ya utekaji yaliyowahi kumkuta.
Nondo ameyabainisha hayo Jijini Dar es salaam mapema leo Mei 23, 2026 wakati akizugumza na waandishi wa habari ambapo mesema Baba Levo amekuwa akitoa kauli hizo kupitia vyombo vya habari, mahojiano pamoja na mitandao ya kijamii, jambo ambalo amesema limemchafua, kumdhalilisha na kuvunja heshima yake mbele ya jamii.
Amesema Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa pamoja na Mahakama Kuu tayari zilishatoa maamuzi yaliyomuondoa hatiani katika kesi iliyokuwa ikimkabili mwaka 2018 kuhusu madai ya kujiteka, huku rufaa ya mwisho iliyowasilishwa Mahakama ya Rufani ikiondolewa mwaka 2022 baada ya upande wa mashtaka kueleza kutokuwa na nia ya kuendelea nayo.
Kupitia wakili wake, Hekima Mwasipu, Nondo amesema tayari wamemtumia Baba Levo notisi ya siku saba wakimtaka kuomba radhi hadharani, kuacha kusambaza taarifa hizo pamoja na kumlipa fidia ya Shilingi milioni 500, vinginevyo watafungua kesi mahakamani.

Comments
Post a Comment