WAZIRI MKUU AAGIZA TADB KUONGEZA UWEZO WA KUFADHILI
Na Mwandishi wetu
WAZIRI Mkuu ameagiza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuongeza uwezo wake wa kifedha ili iweze kufadhili kwa kiwango kikubwa zaidi sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la TADB katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea mkoani Dodoma, Waziri Mkuu amesema benki hiyo imeendelea kuwa chombo muhimu cha Serikali katika kuwawezesha wakulima, wafugaji, wavuvi na wawekezaji kupitia utoaji wa mitaji kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.
Amesema kufikiwa kwa malengo ya taifa ya kuongeza tija katika sekta ya kilimo kunategemea upatikanaji wa mitaji ya kutosha, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuiwezesha TADB ili ikidhi mahitaji yanayoongezeka ya wadau wa sekta hizo.
Amesema kuwa Serikali haiwezi kutegemea ruzuku pekee katika kuendeleza kilimo, hivyo taasisi za kifedha zinapaswa kuwa nguzo muhimu ya uwekezaji kwa kuhakikisha wakulima, wafugaji na wavuvi wanapata mikopo kwa wakati na kwa masharti yanayowawezesha kuongeza uzalishaji.
Waziri Mkuu pia ameitaka TADB kuongeza ufadhili wa ununuzi wa mbolea, pembejeo, zana za kisasa za kilimo na miradi ya kuongeza thamani ya mazao ili kuboresha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, ameitaka benki hiyo kushirikiana na Wizara za Kilimo na Mifugo pamoja na TAMISEMI kuwekeza katika miundombinu ya baada ya mavuno, hususan ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mazao, hatua itakayowezesha wakulima kutumia mazao yao kama dhamana kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imeendelea kufadhili miradi ya kimkakati inayochochea maendeleo ya kilimo, mifugo na uvuvi, ikiwemo kutoa zaidi ya shilingi bilioni 700 kwa miradi ya umwagiliaji pamoja na kusaidia maendeleo ya zao la kahawa kupitia vyama vya ushirika vya mikoa ya Kagera na Kigoma.
Nyabundege amesema TADB pia imefadhili mradi wa kisasa wa ufugaji na uchakataji wa samaki uliopo Bagamoyo unaotumia teknolojia kutoka Misri.



Comments
Post a Comment