KAMPUNI ZA MADINI ZAHIMIZWA KUWA MABALOZI WA MANZINGIRA



Na Wellu Mtaki, Geita

OFISI ya Makamu wa Rais, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mazingira, imeanzisha shindano maalumu linalolenga kuhamasisha kampuni na wachimbaji wa madini kuongeza juhudi katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

Shindano hilo pia linamhusisha Balozi wa Mazingira, Mrisho Mabanzo maarufu kama Mister Tree, katika juhudi za kuhamasisha kampuni, taasisi na jamii kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa agenda ya uhifadhi wa mazingira.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, shindano hilo limewalenga wadau wa sekta ya madini, wakiwemo wachimbaji wadogo pamoja na kampuni kubwa na ndogo zinazojihusisha na shughuli mbalimbali za uchimbaji.

Akizungumza kuhusu mpango huo, mwakilishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais amesema ushirikiano na Balozi wa Mazingira umelenga kutumia ubunifu na njia mbalimbali kuwafikia watu wengi zaidi na kuhamasisha hatua za vitendo katika utunzaji wa mazingira.

Kupitia shindano hilo, kampuni zinazoshiriki zinatakiwa kueleza hatua ambazo zimekuwa zikichukua katika kulinda mazingira, sera walizonazo kuhusu uhifadhi wa mazingira pamoja na namna zinavyoshirikisha jamii katika utekelezaji wa shughuli hizo.

“Lengo ni kuwatambua na kuwahamasisha. Kwa sababu tunasema, kwanza kijifunze, halafu tukutambue au tukupongeze,” amesema mwakilishi huyo.

Amesema shindano hilo litadumu kwa siku nne, ambapo kila kampuni itapata fursa ya kueleza na kuonyesha hatua mbalimbali ilizochukua kuhakikisha shughuli zake zinaendana na misingi ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

Baada ya kukamilika kwa shindano hilo, wadau watakaofanya vizuri wanatarajiwa kutambuliwa na kupongezwa kwa mchango wao katika uhifadhi wa mazingira, huku wakihimizwa kuwa mabalozi na wahamasishaji wa agenda ya mazingira.

kwa Upande wake Stephen Wambura, Afisa wa Usalama na Mazingira kutoka Mamba Mining Company, amesema kampuni hiyo imeweka mkazo katika kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha shughuli zake zinafanyika kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira.

Wambura amesema moja ya maeneo ambayo kampuni hiyo imekuwa ikiyapa kipaumbele ni kuwasaidia wachimbaji wadogo kuendesha shughuli zao kwa usalama na kwa kutumia njia zinazolenga kupunguza athari kwa mazingira.

Amesema matumizi ya kemikali hatarishi, ikiwemo zebaki (mercury), katika shughuli za uchimbaji mdogo yanaweza kusababisha madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.

Kwa msingi huo, amesema Mamba Mining imekuwa ikishirikiana na wachimbaji wadogo kwa kutoa elimu na kuwasaidia kutumia mbinu zinazolenga kupunguza uharibifu wa mazingira unaoweza kusababishwa na shughuli za uchimbaji.

Mbali na hilo, Wambura amesema kampuni hiyo inaendesha kampeni inayojulikana kama “Zero Plastic Campaign”, inayolenga kupunguza matumizi na utupaji holela wa taka za plastiki.

“Plastiki zinaweza kuingia kwenye mitaro na kusababisha madhara mbalimbali. Sisi tunachukua hatua za kukabiliana na tatizo hilo pamoja na kushirikisha jamii inazotuzunguka,” amesema.

Amesema kampuni hiyo pia imekuwa ikifanya uhamasishaji wa mazingira kwa jamii zinazozunguka maeneo ambayo inafanya shughuli zake, kupitia mikutano na programu mbalimbali za elimu ya mazingira.

Kwa mujibu wa Wambura, kampuni hiyo pia imekuwa ikitoa elimu katika shule mbalimbali kwa kuwashirikisha wanafunzi na walimu kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.

Amesema wanafunzi wanaelimishwa ili waweze kuwa mabalozi wa mazingira katika jamii zao na kusaidia kuwahamasisha watu wengine kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.

Wambura amesema Mamba Mining pia imekuwa ikitumia mabango na njia nyingine za mawasiliano kutoa elimu kuhusu namna ya kutunza mazingira katika maeneo mbalimbali.

Kwa ujumla, shindano hilo linatarajiwa kutoa nafasi kwa wadau wa sekta ya madini kuonyesha hatua wanazochukua katika kupunguza athari za shughuli zao kwa mazingira, huku likihamasisha ushiriki mpana wa jamii katika uhifadhi wa mazingira.


Comments

Popular posts from this blog

AWESO ARIDHISHWA NA WINGI WA MAJI RUVU JUU