WMA YAENDESHA ZOEZI LA UHAKIKI MITA ZA UMEME VIWANDANI
Na Mwandishi wetu, DODOMA
WAKALA wa Vipimo (WMA) unaendesha zoezi la kuhakiki mita za umeme zilizofungwa katika viwanda mbalimbali nchini ili kuhakikisha Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inapata mapato stahiki na wenye viwanda wanalipa gharama stahiki kulingana na huduma ya umeme wanaotumia.
Hayo yalibainishwa Juni 18, 2025 na Meneja wa WMA Makao Makuu, Albogast Kajungu wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika uwanja wa Chinangali, Dodoma.
Kajungu amesema kuwa hadi sasa WMA imekagua mita za umeme zaidi ya 2,000 huku lengo likiwa ni kuhakiki mita zote zilizo kwenye matumizi katika viwanda vyote nchini katika zoezi lililoanza Mei mwaka huu.
“Hali inaonesha kwamba mita nyingi zilizo kwenye matumizi viwandani ziko vizuri. Chache ambazo tumekuta zina mapungufu, tumewasiliana na Mamlaka husika kwa ajili ya kuzirekebisha na nyingine kuzibadilisha ili kuhakikisha vipimo viko sahihi kwenye eneo hilo,” amesema Kajungu.
Akieleza zaidi, amesema kuwa zoezi hilo la uhakiki linahusisha mita zote za umeme zilizo katika matumizi lakini Wakala imeona ianze na zile zilizoko viwandani kwakuwa zinatumia umeme mkubwa hivyo ikiwa haziko sawasawa, kuna uwezekano wa TANESCO au wenye viwanda kupata hasara.
Aidha, alieleza kuwa zoezi la uhakiki linahusisha pia bidhaa za chuma hususan zinazotumika katika ujenzi kwani kumekuwa na malalamiko katika eneo hilo.
Akifafanua, Kajungu amesema kuwa sekta ya ujenzi hapa nchini inakua kwa kasi ambapo miradi mingi ya ujenzi inayotekelezwa na serikali inatumia bidhaa za chuma hivyo WMA imeona iongeze nguvu kuhakiki bidhaa hizo hususani zinazozalishwa kwenye viwanda vya ndani ili kuhakikisha zina vipimo vilivyo sahihi.
Amesema. kuwa wazalishaji wanajitahidi kuzalisha kwa kuzingatia viwango lakini lengo la Wakala hiyo ni kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi zinaendelea kuwa na vipimo sahihi ili kuwalinda wananchi dhidi ya madhara ambayo yanaweza kutokea kwa kutumia bidhaa za chuma ambazo hazikidhi vipimo vinavyokubalika kisheria.

Comments
Post a Comment