INEC YAWAHIMIZA WANAWAKE NA VIJANA KUHAKIKISHA USHIRIKI WA WANANCHI KATIKA UCHAGUZI MKUU
Na Mwandishi wetu
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa wito kwa wanawake na vijana nchini kutumia nafasi zao kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Wito huo umetolewa Jijini Dar es salaam mapema leo Julai 31,2025Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji wa Mahakama ya Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk wakati akifungua Mkutano wa INEC na wawakilishi wa wanawake kuelekea uchaguzi mkuu.
Jaji Mborouk amewahimiza wanawake kusambaza taarifa sahihi kuhusu hatua za maandalizi ya uchaguzi na kuwahamasisha wapiga kura waliojiandikisha kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.
“Natoa pongezi kwenu kwa namna mlivyotuunga mkono wakati wote wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Tunawapongeza na tunawashukuru sana,” amesema Jaji Mbarouk,
Kwa upande wake, Mjumbe wa Tume Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari, amewasihi vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa uadilifu na kujiepusha na matumizi yanayochochea chuki au upotoshaji wa taarifa.
“Natoa wito kwenu kuwahamasisha vijana kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na kuepuka mitandao inayosambaza habari za chuki na uchochezi,” amesema
Jaji Asina pia ameonya dhidi ya matumizi mabaya ya teknolojia ya akiliunde (AI), akisisitiza kuwa vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani na kuunga mkono uchaguzi wa haki na wa amani.




Comments
Post a Comment