TPDC YAPATA TUZO YA TAASISI BORA KWA MIAKA MITANO MFULULIZO
Na Mwandishi wetu
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeandika historia kwa kutwaa tuzo ya Taasisi Bora za Umma katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ikiwa ni mara ya tano mfululizo kushinda tuzo hiyo kutokana na ubora wa huduma na uwajibikaji wake kwa wananchi.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TPDC, Maria Mselemu, amesema kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya utendaji kazi bora, nidhamu ya kiutendaji na ufuatiliaji wa karibu wa miradi inayosimamiwa na shirika hilo.
“Hii ni tuzo yetu ya tano mfululizo katika maonesho ya Sabasaba. Ubora wa huduma zetu, miradi ya kimkakati na mchango wetu katika utunzaji wa mazingira umekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio haya,” alisema Mselemu.
Ameongeza kuwa TPDC imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza utoaji wa hewa ukaa kwa kuhimiza matumizi ya nishati safi, hususan kwa matumizi ya majumbani na kwenye magari. “Tayari tumeondoa zaidi ya tani 100,000 za hewa ukaa kupitia juhudi zetu za kusambaza gesi asilia. Ni mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,” amesema
TPDC pia imewahi kutwaa tuzo ya mazingira kutokana na juhudi zake katika kulinda na kuhifadhi mazingira kupitia matumizi ya nishati mbadala, jambo linaloendelea kuipa heshima shirika hilo miongoni mwa taasisi za umma.
Maonesho ya Sabasaba yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuonesha ubunifu, huduma na bidhaa bora kwa Watanzania, huku yakitoa fursa kwa mashirika kama TPDC kushirikiana na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi.




Comments
Post a Comment