KABIRIGA AWAHIMIZA WANANCHI UKONGA KUMUAMINI: "NAKUJA KUONDOA KERO ZOTE"
- Get link
- X
- Other Apps
Na Mwandishi Wetu
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Ukonga kupitia Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Murshid Kabiriga, amewataka wananchi wa jimbo hilo kumpa ridhaa ya kuwaongoza kwa kuwa ana nia thabiti na mipango madhubuti ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Akizungumza na mara baada ya kurejesha fomu Kabiriga amesema Ukonga inakabiliwa na changamoto nyingi, hususan miundombinu mibovu ya barabara na uhaba wa miundombinu ya elimu.
"Jimbo la Ukonga tumepata kata moja tu yenye barabara, kata zilizobaki hazina. Sasa ninasema hapana, nawaomba wananchi waniamini, nina nia njema na naenda kupambana kuhakikisha tunaleta maendeleo," amesema
Kabiriga alibainisha kuwa shule nyingi za msingi na sekondari ndani ya jimbo hilo bado hazina madawati ya kutosha na wanafunzi hulazimika kukaa chini, jambo ambalo alisema linapaswa kutafutiwa ufumbuzi wa haraka.
"Ninafahamu changamoto zote kwa sababu mimi ni mzaliwa wa Ilala na najua vizuri Ukonga. Wananchi wananijua na hata kabla ya kugombea nimekuwa nikitatua matatizo kadhaa. Sasa nataka kwenda kufanya kazi kubwa zaidi kupitia nafasi ya Ubunge," alisema Kabiriga.
Amesema iwapo atapewa dhamana hiyo, atahakikisha anashirikiana na wananchi katika kuondoa kero za muda mrefu ikiwemo miundombinu duni, uhaba wa huduma za jamii na kuinua hali ya maisha ya wakazi wa Ukonga.
"Tuungane kwa pamoja kuibadilisha Ukonga. Mimi nina nia, uwezo na maono ya kuleta maendeleo ya kweli," amesisitiza
- Get link
- X
- Other Apps

Comments
Post a Comment