MGOMBEA UBUNGE ILALA KUPITIA CUF AHAIDI KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANANCHI

 




Na Mwandishi Wetu

MGOMBEA wa Ubunge wa Jimbo la Ilala kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Mary Majani amesema ana nia, uwezo na nguvu ya kuwatumikia wananchi wa Ilala, huku akiahidi kupambana kwa nguvu zote kutatua changamoto zinazowakabili wakazi wa jimbo hilo, hususan vijana na wajasiriamali.

Akizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam Agosti 26,2025 mara baada ya kurejesha fomu ya kugombea, Mary amesema ameamua kugombea nafasi hiyo kwa kuwa anafahamu kwa undani matatizo ya wananchi wa Ilala, hasa vijana wasiokuwa na ajira na mazingira magumu wanayopitia wajasiriamali katika maeneo ya masoko na biashara ndogondogo.

“Mimi ni mwanamke, na mwanamke anajua uchungu wa nchi yake na wa watoto wake. Vijana wetu wa Ilala hawana kazi, masoko yapo lakini mazingira ni magumu kwa wajasiriamali. Nikipewa ridhaa, nitakuwa sauti ya kuwatetea bungeni,” alisema Mary.

Ameongeza kuwa moja ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha Ilala inakuwa na huduma bora za afya, upatikanaji wa maji safi na salama, pamoja na kuwianisha maendeleo katika maeneo yote ya jimbo hilo.



“Ninawaomba wananchi wa Ilala wanikabidhi dhamana. Nitashirikiana nao bega kwa bega kuleta mabadiliko na maendeleo ya kweli,” amesema Mary

Mary ameahidi kuwa akichaguliwa, atahakikisha kila mwananchi anapata fursa ya kusikilizwa, na kuwa kiongozi atakayekuwa karibu na watu wake wakati wote.

Comments

Popular posts from this blog

WANAFUNZI WALIOMALIZA KIDIA SEKONDARI WACHANGIA UJENZI WA KANISA SH MILLION 20

VETA YAJIPANGA KUSHIRIKINA NA TOYOTA TANZANIA KUIMARISHA MAFUNZO YA UFUNDI MAGARI

UJENZI WA BWAWA LA KUFUA UMEME LA MTO MALAGARASI , WAPIGA HATUA MPYA