MKUTANO WA WAKUU WA TAASISI ZA UMMA KUCHOCHEA MAGEUZI NA USHINDANI




Na Mwandishi wetu

KATIKA kuendeleza juhudi za Serikali kuhakikisha taasisi za umma zinakuwa sehemu hai ya uchumi wa kisasa, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeandaa kikao kazi maalum ‘CEO Forum 2025’ kitakachowaleta pamoja Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa mashirika ya umma nchini wapatao 700.

Mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Agosti 23-26 jijini Arusha, unalenga kujadili kwa kina jinsi taasisi za umma zinavyoweza kuwa shindani katika soko la kimataifa, kuongeza mapato yasiyo ya kodi, na kushiriki kikamilifu katika kuendesha uchumi wa kisasa unaoongozwa na matokeo.

Kupitia mijadala ya kitaasisi, Serikali inalenga kuimarisha ufanisi, uwajibikaji na ubunifu katika taasisi hizi ili ziweze kuwa wabia halisi wa maendeleo ya Taifa.

Aidha, akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumatatu, Agosti 11, 2025,  Lightness Mauki, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini—Mashirika ya Umma ya kibiashara, alisema kipaumbele kitawekwa katika kufanikisha utekelezaji wa Dira 2050, kwa kuhakikisha taasisi za umma zinajipanga kuwa wabia wa kweli wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.



Kwa mujibu wa Dira 2050, Serikali imedhamiria kuwa na uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050, huku pato la Taifa likifikia $1 trilioni na pato la mtu mmoja mmoja $7000 kwa mwaka.

Mauki alisema ili kufikia matamanio hayo ni lazima kujenga misingi imara ya ushirikiano kati ya vyombo vya maamuzi na wasimamizi wa utekelezaji ndani ya taasisi za umma, ili kuongeza tija, uwajibikaji na uwezo wa kushindana katika mazingira ya kikanda na kimataifa.



Ni katika muktadha huo, katika kipindi ambacho dunia inakumbwa na mabadiliko ya haraka ya kiuchumi, kiteknolojia na kisera, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imetambua haja ya kuwa na jukwaa mahsusi la kujadili, kutathmini na kuimarisha mwelekeo wa pamoja wa taasisi zake za umma – ndipo likazaliwa wazo la CEO Forum miaka mitatu iliyopita.

Comments

Popular posts from this blog

WANAFUNZI WALIOMALIZA KIDIA SEKONDARI WACHANGIA UJENZI WA KANISA SH MILLION 20

VETA YAJIPANGA KUSHIRIKINA NA TOYOTA TANZANIA KUIMARISHA MAFUNZO YA UFUNDI MAGARI

UJENZI WA BWAWA LA KUFUA UMEME LA MTO MALAGARASI , WAPIGA HATUA MPYA