AICC YAJIPANGA KUIMARISHA HUDUMA ZA MIKUTANO, YATOA WITO KWA WADAU KUJITOKEZA

 



Na Mwandishi Wetu

KITUO cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) kimesema kimeendelea kuboresha miundombinu na huduma zake za mikutano, kikilenga kuwahudumia wadau wa ndani na wa kimataifa huku kikichangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 26, 2025 na Ofisa Mawasiliano na Uhusiano wa AICC, Mourine Kaaya, wakati wa maonesho ya 22 ya Wahandisi yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Kaaya amesema kuwa pamoja na kuendesha mikutano ya kimataifa, AICC pia linatoa huduma kwa shughuli mbalimbali za kijamii kama harusi, semina, warsha na hafla nyingine, kupitia kumbi zake mbalimbali, ikiwemo Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC).

“AICC imekuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa, pia kwa wananchi mmoja mmoja kutokana na wageni wanaokuja kwenye kumbi hizi na kufanya mikutano, ambao huhitaji huduma nyingine kama malazi, usafiri na chakula,” amesema Kaaya.




Amesema huduma hizo zimekuwa zikinufaisha wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Arusha, ambako ndiko yaliko makao makuu ya AICC na JNICC, kwa kuongeza kipato kupitia biashara ndogondogo na ajira zisizo rasmi.

Kaaya ameongeza kuwa kumbi hizo zimeendelea kuwa kivutio kutokana na mazingira ya kuvutia na miundombinu ya kisasa, hali inayowavutia wadau wengi wa sekta mbalimbali kuendesha shughuli zao katika maeneo hayo.


“Tunawakaribisha wadau wote kukodi kumbi zetu kwani hatujihusishi na mikutano ya kimataifa tu bali tunatoa huduma pia kwa mikutano ya ndani na shughuli mbalimbali za kijamii,” amesema.





Comments

Popular posts from this blog

WANAFUNZI WALIOMALIZA KIDIA SEKONDARI WACHANGIA UJENZI WA KANISA SH MILLION 20

VETA YAJIPANGA KUSHIRIKINA NA TOYOTA TANZANIA KUIMARISHA MAFUNZO YA UFUNDI MAGARI

UJENZI WA BWAWA LA KUFUA UMEME LA MTO MALAGARASI , WAPIGA HATUA MPYA