DKT. BITEKO AELEZA MIAKA 10 YA MAPINDUZI YA MAENDELEO BUKOMBE,



Ataja sababu za kumchagua Dkt. Samia kwa kura nyingi

NA MWANDISHI WETU

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Bukombe kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto Mashaka Biteko amesema kuwa kwa Serikali ya CCM inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Wilaya ya Bukombe ikiwa ni pamoja na kutoa fursa za kukuza uchumi wa Wilaya hiyo.

Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 27, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Katente wilayani Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Amesema mwaka 2015 Kata ya Katente, Igulwa na Kata zote zilizopo maeneo ya mjini zilikuwa na kiwango duni sana cha maendeleo ikilinganishwa na maendeleo yaliyofikiwa sasa.


Amesema Wilaya ya Bukombe ilikuwa na shule moja ya kidato cha tano na sita, hospitali moja, zahanati nne huku umeme ukiwa katika vijiji saba pekee.

Amesema Serikali ya CCM imekuwa ikifanya jitihada kubwa ya kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuboresha maisha ya wananchi wa Wilaya hiyo ambapo sasa inajenga jengo la Ofisi ya Mkuu Wilaya, jengo la halmashauri, soko na stendi ya kisasa.

“ Rais samia ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Ushirombo kwenda Katoro kwa kiwango cha lami ambao unaendelea na ameruhusu watu kuchimba dhahabu katika Pori la Kigosi na sasa vijiji vyote vimepelekewa umeme,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu mbalimbali “ Tunajenga Chuo cha VETA pamoja na Chuo Kikuu vyote hivi vitasaidia kuleta mzunguko wa fedha na kukuza uchumi wetu, watu hawataki maneno wanataka maendeleo na Dkt. Samia amedhamiria kuibadilisha Bukombe,”

Sambamba na hayo, Dkt. Biteko amewahimiza wananchi wa Katente 19,000 waliojiandikisha kupiga kura ifikapo Oktoba 29 wamchague Dkt. Samia kwa nafasi ya Urais, mbunge na diwani wa CCM ili kuendelea kuchochea maendeleo ya Wilaya ya Bukombe.

Comments

Popular posts from this blog

WANAFUNZI WALIOMALIZA KIDIA SEKONDARI WACHANGIA UJENZI WA KANISA SH MILLION 20

VETA YAJIPANGA KUSHIRIKINA NA TOYOTA TANZANIA KUIMARISHA MAFUNZO YA UFUNDI MAGARI

UJENZI WA BWAWA LA KUFUA UMEME LA MTO MALAGARASI , WAPIGA HATUA MPYA