DKT. BITEKO KUFANYA MAKUBWA KATA YA BUGELENGA,
Asema watakaounganishiwa umeme kupewa majiko
Na Mwandishi wetu
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu. Doto Mashaka Biteko amewapongeza wananchi wa Kata ya Bugelenga, Wilaya ya Bukombe kwa kushirikiana na kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Kata yao ikiwemo ujenzi wa shule, barabara na miradi ya maji.
Ametaja moja ya mradi kuwa ni ujenzi barabara ya Bufanka – Ikalanga hadi Bukombe ambapo ameahidi kuwa CCM ikipewa dhamana ya kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano, itatekeleza miradi zaidi ili kuwaletea maendeleo wananchi kwa kukabiliana na kero zinazowakabili.
Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 20, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Bugelenga wilayani Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imefikisha umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo vijiji sita vya Kata ya Bugelenga na kazi iliyobaki ni kupeleka umeme katika vitongoji tisa vya Kata hiyo.
Amewaeleza wananchi kuwa CCM itaendelea kusogeza huduma bora za jamii ambapo ameahidi kuwa kuanzia sasa wananchi wakiunganisha umeme watapewa majiko ya umeme bure ikiwa ni njia ya kupunguza gharama ya kupikia ikilinganishwa na matumizi ya kuni.
Dkt. Biteko pia amesema watajenga kituo kikubwa cha kupooza umeme ili kuweza kusambaza umeme huo hadi Mbogwe, watajenga madarasa, maabara na jengo la utawala.
“ Mgombea udiwani ameeleza kuhusu shule zinazohitaji ukarabati hivyo ni lazima zikarabatiwe katika kipindi kinachokuja. Pia,
Nataka niwaambie tutajenga wodi kwa ajili ya kulaza wagonjwa katika Kata hii,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo CCM imedhamiria kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuongeza miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa maji.
Kuhusu umuhimu wa elimu, amewaasa wananchi hao kuwasomesha watoto wao kwa kuwa Serikali imeendelea kulipa ada kwa wanafunzi wote kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha sita. @biteko @ccmtanzania

Comments
Post a Comment