MAABARA ZA MADINI ZAHIMIZWA KUTUMIA CRUCIBLE ZA GST

 


Na Mwandishi wetu, GEITA

MAABARA mbalimbali nchini  zinazojishughulisha na uchunguzi wa sampuli za madini zimehimizwa kutumia vikombe vya kuyeyushia sampuli zenye madini ya dhahabu (Crucible) zinazotengenezwa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili kuongeza tija kwenye uchunguzi wa sampuli za madini ya dhahabu kwa njia ya tanuru (fire assay).

Hayo yamesemwa leo, tarehe 25 Septemba 2025, na Gideon Nshange ambaye ni  Fundi Sanifu Mkuu GST, wakati akizungumza na wadau mbalimbali  wanaotembelea banda la GST katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili, mkoani Geita.

Akielezea sifa za vikombe hivyo, Nshange amesema kuwa, vikombe hivyo  vina ubora wa hali ya juu, unaochangiwa na uwezo wake wa kuhimili joto kali hadi kufikia nyuzi joto 1400.

Sambamba na hapo ameongeza kuwa, vikombe hivyo vinaokoa gharama za uendeshaji kwani vina uwezo wa kuyeyushia sampuli zenye madini ya dhahabu kwa zaidi ya mizunguko mitatu.

Nshange amefafanua kuwa,  kutokana na ubora huo, mwitikio wa wateja umekuwa umeendelea kuwa mkubwa siku baada ya siku ambapo asilimia kubwa walioanza kutumia  sasa wamekuwa wateja wa kudumu.

GST imekuwa ikizalisha vikombe hivyo katika ujazo tofauti ukianzia D60 mpaka D65 kwa matumizi ya ndani pamoja na wateja wa nje kwa takribani miaka 15 sasa.

Comments

Popular posts from this blog

WANAFUNZI WALIOMALIZA KIDIA SEKONDARI WACHANGIA UJENZI WA KANISA SH MILLION 20

VETA YAJIPANGA KUSHIRIKINA NA TOYOTA TANZANIA KUIMARISHA MAFUNZO YA UFUNDI MAGARI

UJENZI WA BWAWA LA KUFUA UMEME LA MTO MALAGARASI , WAPIGA HATUA MPYA