MFUMO WA DIJITALI KUTUMIKA KUKUSANYA TAARIFA ZA MATUKIO YA WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU



Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imekuja na mkakati wa kupata taarifa sahihi na kwa haraka kupitia Mfumo wa Kieletroniki wa Ukusanyaji wa Taarifa za Matukio ya Wanyamapori Wakali na Waharibifu (Problem Animals Information System – PAIS) ili kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi za matukio ya wanyama hao kwa haraka 

Akifungua mafunzo ya mfumo huo kwa Maafisa Ugani 120 Jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Alexander Lobora, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori  amesema kuwa  lengo la Serikali kuhifadhi rasilimali  za wanyamapori ni kuleta maendeleo  kwa Taifa  na ustawi wa wananchi wake na si kugeuka kuwa mzigo kwa jamii. 

“Miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na matukio ya mara kwa mara ya wanyamapori wakali na waharibifu ambayo imepelekea madhara kwa wananchi na mali zao ikwemo majeruhi, vifo, uharibifu wa mazao,  miundombinu na vifo vya mifugo.’’ alisema Dkt. Lobora

Amesisitiza kuwa kwa  sasa Wizara imekuja na mkakati wa matumizi ya teknolojia kuhakikisha inapata taarifa sahihi na kwa haraka kupitia mfumo wa kidijitali ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu ulipaji wa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wakati. 

Awali,  Kay Kagaruki, Mkurugenzi Msaidizi Matumizi ya Wanyamapori kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori alisema kuwa, juhudi za Serikali katika uhifadhi wa rasilimali za maliasili wakiwemo wanyamapori zinaungwa mkono na wadau mbalimbali hata hivyo hivyo, amesisitiza kuwa uhifadhi wa wanyamapori bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo migongano baina ya binadamu na wanyamapori, ujangili wa wanyamapori. 

“Katika kuimarisha utatuzi wa changamoto hizo, Wizara imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuandaa Mfumo wa kielektroniki wa kukusanya na kuchakata taarifa ya matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu uwandani (Problem Animals Information System-PAIS) ili kuharakisha utoaji wa taarifa hizo kwa ajili ya udhibiti na ulipaji wa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wakati. “ alisema Kagaruki

Naye Theodory Mulokozi, Afisa Mazingira  Mwandamizi OR- TAMISEMI, aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kuandaa mafunzo hayo na kutoa vitendea kazi kwa ajili ya ukusanyaji wa taarifa husika na kutoa  wito kwa Maafisa Ugani kutumia vitendea kazi walivyokabidhiwa kwa kazi iliyokusudiwa na si vinginevyo.

Comments

Popular posts from this blog

WANAFUNZI WALIOMALIZA KIDIA SEKONDARI WACHANGIA UJENZI WA KANISA SH MILLION 20

VETA YAJIPANGA KUSHIRIKINA NA TOYOTA TANZANIA KUIMARISHA MAFUNZO YA UFUNDI MAGARI

UJENZI WA BWAWA LA KUFUA UMEME LA MTO MALAGARASI , WAPIGA HATUA MPYA