MGOMBEA URAIS TLP AAHIDI MAGEUZI YA KIUCHUMI, ELIMU NA AFYA.



Na Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM 

MGOMBEA wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Mbatina Rwamugira
amewaomba Watanzania kumpa ridhaa ya kuongoza nchi kwa miaka mitano ili kuleta mageuzi ya kiutawala, kiuchumi, elimu na afya.

Rwamugira amebainisha hayo  Jijini Dar es salaam Septemba 4,2025 katika uzinduzi wa Kampeni za Chama hicho kuelekea uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Octoba 29,2025 .
Amesema Tanzania ni nchi ya amani tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na kwamba ataendeleza amani hiyo sambamba na kutekeleza mahitaji ya wananchi kwa ufanisi na utulivu.

“Nchi hii ni ya amani. Mkinipa uongozi, nitaendesha kwa utulivu, nikitekeleza kazi zenu wananchi kwa moyo wa dhati,” alisema.

Alieleza kuwa serikali ya TLP imedhamiria kuimarisha utawala bora, kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, na kuanzisha viwanda vidogo vidogo katika kila mkoa ili kuchochea ajira na kukuza uchumi wa ndani.

Aliahidi kuwa vijana watakaokosa ajira rasmi, watawezeshwa kwa kuanzishiwa viwanda vya uzalishaji na kupewa mazingira bora ya kujiajiri.

Kuhusu elimu, alisema Elimu kuanzia chekechea hadi chuo kikuu itakuwa bure kupitia mfumo wa mikopo rafiki.Kila shule ya sekondari itatoa mafunzo ya ufundi kama kilimo na maabara.




Katika sekta ya afya, aliahidi huduma bure kwa wananchi wote na kuhakikisha kila Mtanzania anapata bima ya afya

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kutoshiriki kwenye vurugu wala kejeli wakati wa kampeni na uchaguzi, akihimiza utulivu na mshikamano.

 “Tusisusie uchaguzi. Tujitokeze kwa wingi kupiga kura kwa amani,” alisisitiza.

Aidha  amesisitiza kuwa TLP iko tayari kuleta maendeleo ya kweli na kumtumikia Mtanzania kwa uadilifu.


Comments

Popular posts from this blog

WANAFUNZI WALIOMALIZA KIDIA SEKONDARI WACHANGIA UJENZI WA KANISA SH MILLION 20

VETA YAJIPANGA KUSHIRIKINA NA TOYOTA TANZANIA KUIMARISHA MAFUNZO YA UFUNDI MAGARI

UJENZI WA BWAWA LA KUFUA UMEME LA MTO MALAGARASI , WAPIGA HATUA MPYA