OTHMAN MASOUD: UCHAGUZI WA OKTOBA 29 NI FURSA YA KUIKOMBOA ZANZIBAR
NA MWANDISHI WETU
MKUTANO mkubwa wa kampeni za ACT Wazalendo umefanyika katika viwanja vya Mpapa, Wilaya ya Kati Unguja, ambapo maelfu ya wananchi walijitokeza kumuunga mkono Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, Othman Masoud Othman huku Meneja wa kampeni Ismail Jussa akiibua sakata zito la ufisadi kwenye ununuzi wa magari 150.
Akizungumza katika mkutano huo, Ismail Jussa, aliweka wazi sakata zito la ufisadi lililotokea mwaka 2023, ambapo Serikali ilihusishwa na ununuzi wa magari 150 kwa gharama ya shilingi bilioni 17 kupitia kampuni ya FK Motors kutoka Dar es Salaam.
Alifafanua kuwa kampuni hiyo haikuwa na uwezo wa kifedha na ilipewa mkopo wa shilingi bilioni 12 na Benki ya PBZ, kisha Serikali ya Zanzibar ikajidhamini yenyewe kupitia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais.
Jussa alisema magari hayo hayakuwa mapya bali yaliyokwisha tumika, huku gharama halisi za ununuzi zikiongezewa na kodi ya VAT kutozwa kinyume cha sheria, fedha ambazo zilielekezwa kwa mtu mmoja pekee. “Huu ni ufisadi wa kutisha uliotengenezwa na watawala wachache kwa maslahi yao binafsi huku wananchi wakiendelea kubaki maskini,” alisema Jussa.
Aidha, aliongeza kuwa kwa miaka mitano ya utawala uliopo madarakani, Wazanzibari hawajafaidika na chochote cha maana.
Alisema ahadi za ajira hazijatekelezwa huku vijana wakipumbazwa kwa maneno matupu.
“Wanatuambia wataleta ajira laki tatu na hamsini wakati hata ahadi ya ajira laki tatu za awamu iliyopita haikutimizwa. Vijana wa Zanzibar hawahitaji kuendelea kudanganywa, wanahitaji misingi ya kielimu na ajira za kweli zitakazowajengea thamani,” alisisitiza.
Jussa pia alibainisha kuwa Serikali iliyopo madarakani imeongeza mshahara kwa shilingi elfu 50 pekee katika kipindi cha miaka mitano, huku wakiweka bima ya afya inayowakatia wafanyakazi shilingi elfu 80 kila mwezi, jambo ambalo limezidisha mzigo badala ya kuleta nafuu.
Kwa upande wake, Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, aliwaeleza wananchi kuwa uchaguzi wa Oktoba 29 ni wa kihistoria na wa kipekee, kwani utakuwa ni nafasi ya kuikomboa Zanzibar kutoka mikononi mwa dhulma na ufisadi wa watawala waliopo.
Uchaguzi huu ni wakuinusuru Zanzibar. Baada ya Wazanzibari kufaidika matunda ya Mapinduzi, sasa wanachofanyiwa ni kudhulumiwa kwa jina la Mapinduzi yenyewe. Afya bora, elimu bora, na maisha mazuri yalipaswa kuwa matunda ya Mapinduzi, lakini zaidi ya miaka 60 hali bado ni duni.
Ni wakati wa Wazanzibari kufanya maamuzi magumu na sahihi kwa mustakabali wa kizazi kijacho,” alisema Othman kwa msisitizo.
Othman aliongeza kuwa katika miaka yote aliyohudumu Serikalini hajawahi kuhusishwa na kashfa yoyote ya kifisadi.
Alisema jambo pekee lililomfanya akosane na watawala ni msimamo wake wa kuitetea Zanzibar, akiamini kwa dhati kuwa nchi hiyo inapaswa kuwa huru na kujitawala bila kuburuzwa.
Katika hoja yenye uzito mkubwa, Othman alisema ni jambo la kusikitisha kuona wananchi wa Zanzibar wanaendelea kufanywa kama watumwa katika nchi yao wenyewe. Alieleza kuwa hali hiyo inatokana na uongozi usiojali maslahi ya wananchi, bali maslahi ya kikundi kidogo cha watu wachache wanaonufaika na utawala wa sasa.
Alisisitiza kuwa Wazanzibari wanapaswa kusimama kidete kudai heshima yao na kulinda utu wao, kwani hakuna mtu atakayeikomboa Zanzibar isipokuwa wananchi wenyewe kupitia kura zao.
Wananchi waliohudhuria mkutano huo pia walitoa maoni yao kwa nguvu kubwa za ushawishi.
Asha Suleiman, mkazi wa Bungi, alisema: “Tumechoshwa na ahadi za uongo. Vijana wetu hawana ajira, kila siku ni umasikini. Tunamuona Othman Masoud kama tumaini jipya litakaloleta haki na maendeleo.”
Kwa upande wake, kijana Hamad Ali kutoka Kati alisema: “Serikali imekuwa ikituchezea kwa miaka mingi. Hatuwezi tena kukaa na kusubiri ajira za kuahidiwa.
Tunataka mabadiliko na ndio maana tumekuja kwa wingi kuunga mkono ACT Wazalendo.”
Naye Mzee Abdalla Hassan, mstaafu kutoka Jendele, aliongeza: “Baada ya Mapinduzi tuliamini tutapata maisha bora, lakini mpaka leo bado hali ni mbaya. Hii ni mara yetu ya mwisho kuikomboa Zanzibar na kurejesha heshima ya wananchi.”
Mkutano huo umeacha taswira kubwa ya hamasa na mshikamo wa wananchi, huku ACT Wazalendo ikionekana kupata mwamko mpya wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
Imetolewa na Idara ya Habari na Uenezi
ACT Wazalendo
24 Septemba 2025


Comments
Post a Comment