SHEN MARATHON 2025 KUKWAMUA MTOTO WA KIKE KIELIMU
Na Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM.
KATIKA juhudi za kumkomboa mtoto wa kike kiuchumi na kielimu, Chuo cha City Institute of Health cha jijini Dar es Salaam kimetangaza kuandaa mbio maalum za SHEN MARATHON 2025, zitakazofanyika Oktoba 25, 2025, katika viwanja vya Leaders Club.
Akizugumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Septemba 27, 2025, mwamuzi wa kike wa mpira wa miguu nchini, Elizabeth Ntungu, amesema kuwa lengo kuu la mbio hizo ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwalipia ada wanaosomea kazi za afya ngazi ya Diploma, ambao wanakumbwa na changamoto za kifedha
"Tunatambua kuwa mtoto wa kike akipewa nafasi ya kusoma, analeta manufaa makubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla. Ndiyo maana tumelenga kuwawezesha zaidi ya wasichana 100 wanaosomea fani za udaktari, uuguzi, ufamasia na kozi nyingine za afya," amesema Ntungu.
Amesema kuwa SHEN MARATHON 2025 ni harakati ya kuwekeza katika mustakabali wa taifa kwa kuwaelimisha wasichana ambao baadaye watakuwa sehemu ya nguvu kazi katika sekta ya afya.
Ntungu ambaye pia ni mwanzilishi wa SHEN MARATHON 2025 ametoa wito kwa wananchi wote, vikundi vya jogging, taasisi za umma na binafsi, watu maarufu pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ya elimu na afya kujitokeza kwa wingi kushiriki au kuchangia kwa namna yoyote ile mbio hizo.
"Tunawaomba Watanzania wote kwa ujumla wajitokeze kwa wingi kushiriki au kusaidia mbio hizi, ili kuhakikisha wasichana hawa wanatimiza ndoto zao na kuja kulitumikia Taifa kwa ufanisi," amesema.
Kwa upande wake, Balozi wa SHEN MARATHON 2025, Paschalia Silanda, amesema kuwa mbio hizo ni sehemu ya juhudi za kumsaidia mwanamke na msichana ambaye amekumbana na changamoto mbalimbali za kimaisha zikiwemo ukosefu wa ada na mazingira magumu ya kujifunza.
"Mwanamke ni mtu anayepitia changamoto nyingi katika jitihada za kujikwamua kiuchumi au kutimiza ndoto zake. Kupitia SHEN MARATHON 2025, ataweza kupata nafasi ya kurudi shuleni na kuijenga kesho yake," amesema Silamda.
Naye Mkuu wa Chuo cha City Institute of Health, Nuran Mwasha, amesema lengo kuu ni kuinua mtoto wa kike aliyekumbana na changamoto ya kushindwa kumaliza masomo kutokana na ukosefu wa ada.
"Mbio hizi zimebeba ujumbe mkubwa wa matumaini kwa wasichana wengi waliokwama kielimu. Ushiriki wa kila mmoja wetu ni mchango katika mustakabali wa taifa," amesema Mwasha.
Naye Dkt. Mohamed Hamis, mdau wa soka na elimu, amesema kuwa SHEN MARATHON 2025 ni mbio za kwanza za aina yake ambazo kwa makusudi zimeelekezwa kumsaidia mtoto wa kike, akisisitiza kuwa kuwekeza kwa mwanamke ni sawa na kuwekeza kwa jamii nzima.
"Ukimkomboa mwanamke, umeikomboa jamii nzima. Hii ni fursa adhimu kwa kila mmoja wetu kushiriki katika kuandika historia ya mafanikio ya wasichana nchini," amesisitiza Dkt. Hamis.






Comments
Post a Comment