UJENZI WA BARABARA ZA LAMI KUKUZA UCHUMI WA WANANCHI TANGANYIKA
Na Mwandishi wetu, TANGANYIKA KATAVI
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ndugu Ismail Ali Ussi, ameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) Mkoa wa Katavi kwa kutekeleza ujenzi wa barabara za kiwango cha lami za Mji wa Majalila Wilaya ya Tanganyika Mkoani humo zenye urefu wa km 4.0 huku zikitajwa kuwa chachu ya ustawi wa maendeleo ya watu kiuchumi na jamii
Awali akisoma taarifa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 Ismail Ali Ussi, Meneja wa TARURA Wilaya ya Tanganyika Mhandisi. Nolasco Kamasho amesema mradi wa barabara za Mji wa Majalila uliojengwa Kijiji cha Majalila Kata ya Tongwe una urefu wa km 4.0 na umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.862
Mhandisi huyo amesema utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa barabara hizo unatokana na fedha za Mfuko wa Barabara, hivyo kama TARURA walikuwa na jukumu la kuhakikisha ujenzi wa barabara unakamilika kwa wakati na ukiendana na thamani halisi ya fedha.
Aidha, mkazi wa Mji wa Majalila Maria Shija amesema barabara hizo zitawasaidia kufika kwa haraka katika huduma za kijamii kama vile vituo vya afya na kuondoa adha ya usafirishaji wa mazao na bidhaa mbalimbali kutoka mashambani na kuyafikisha kwenye masoko



Comments
Post a Comment