CHALAMILA AMKABIDHI MJANE ALICE HAULE HATI YA NYUMBA
Na Mwandishi wetu
SERIKALI kupitia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, imemkabidhi rasmi hati ya umiliki wa nyumba Alice Haule, mjane wa marehemu Justus Rugaibura, kufuatia uamuzi wa Tume Maalum ya Serikali uliohitimisha mgogoro wa muda mrefu na mfanyabiashara Mohamed Yusufali.
Makabidhiano hayo yamefanyika Oktoba 20, 2025, ambapo Alice pia alipokea Shilingi Milioni 10 kama mtaji wa kuanzisha maisha mapya baada ya kipindi kigumu cha mapambano ya haki.
Akizungumza katika hafla hiyo, Chalamila amesema hatua hiyo imefuatia uchunguzi wa kina uliofanywa na Wizara ya Ardhi, ambapo ilibainika kuwa mikataba ya mauziano kati ya marehemu Rugaibura na Yusufali haikuwasilishwa rasmi wizarani kama sheria inavyotaka.
"Huu ni ushahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kusimamia haki za wananchi na kupigania wanyonge,” amesema Chalamila.
Akiwasilisha ripoti hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Kamishna Msaidizi wa Ardhi, Shukurani Kyando, amesema timu ya uchunguzi ilipitia nyaraka, kuwahoji wahusika na kufuatilia mwenendo mzima wa umiliki, kabla ya kufikia uamuzi.
Kwa upande wake Alice Haule aliishukuru Serikali kwa kuweza kumpigania na hatimaye kupata haki yake
“Namshukuru sana Rais Samia kwa kunitetea. Naomba wananchi wengine waendelee kuiamini Serikali yao. Haki ipo, tusikate tamaa.”





Comments
Post a Comment