CHALAMILA: MABADILIKO YA TABIANCHI NI ADUI MPYA WA TAIFA
Asisitiza matumizi ya umeme wa kupikia kama suluhisho endelevu
Na Mwandishi wetu
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema kuwa ajenda ya matumizi ya nishati safi, hususani umeme katika shughuli za upishi, ni mpango mkubwa wa kitaifa unaolenga kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi ambayo sasa ni tishio kubwa kwa taifa.
Chalamila ametoa kauli hiyo mapema leo Octoba 9,2025jijini Dar es Salaam wakati akizindua programu ya “Konekti Umeme, Pika kwa Umeme” iliyoandaliwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kushirikiana na kampuni ya MEXI pamoja na wadau wa maendeleo kutoka Serikali ya Uingereza kupitia UKAID.
Amesema mabadiliko ya tabianchi yamesababisha ukosefu wa mvua, kuharibu vyanzo vya maji na umeme, na kuongeza magonjwa, njaa na ukame. Kwa mujibu wake, tatizo hilo haliwezi kushughulikiwa kwa silaha, bali kwa elimu na utekelezaji wa ajenda ya nishati safi.
"Zamani tulijua adui ni yule anayeweza kushikwa kwa bunduki, leo tunamgundua adui mkubwa zaidi ni mabadiliko ya tabianchi. Adui huyu halindwi kwa silaha bali kwa elimu na utekelezaji wa ajenda ya nishati safi,” amesema Chalamila.
Ameongeza kuwa Dar es Salaam ni soko kubwa la mkaa unaokatwa mikoani, hivyo wakazi wake wanapaswa kuwa mstari wa mbele kukataa matumizi ya nishati hiyo chafu ili kulinda mazingira na afya za vizazi vijavyo.
“Mkaa unakatwa mikoani, lakini soko lake ni Dar es Salaam. Mkisema hapana, biashara ya ukataji miti itakufa. Mkikumbatia nishati safi, mnaponya mazingira ya nchi,” amesema
Katika hatua nyingine Chalamila aliipongeza TANESCO kwa kuanzisha mpango unaowawezesha wananchi kupata majiko ya umeme kwa mkopo kupitia bili zao za umeme, hatua aliyosema inatoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.
“Ajenda hii inalinda afya za kina mama wanaopika, inalinda ndoa, inalinda mazingira, na zaidi inalinda uchumi wa taifa,” amesema
Aidha aliwataka viongozi wa serikali za mitaa kushirikiana kikamilifu katika kuelimisha wananchi juu ya faida za matumizi ya nishati safi kwa mustakabali wa taifa, akisisitiza kuwa hili si suala la chama, kabila wala jinsia, bali ajenda ya kitaifa.
“Leo ni TANESCO mtaani kwako, kesho ni wewe katika familia yako. Pika kwa umeme, linda afya yako, linda mazingira yako, linda amani ya taifa lako,” amesisitiza
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema shirika hilo limeanza kusambaza majiko ya umeme kwa mkopo siyo tu kwa wafanyakazi wake, bali sasa kwa wananchi wote kupitia mpango wa kulipa kidogo kidogo kupitia bili za umeme.
Twange amesema kuwa mpango huo umeondoa kikwazo cha gharama za awali na kufungua milango kwa kaya nyingi kuingia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Comments
Post a Comment