ELIMU YA USALAMA NA AFYA KAZINI YAWAFIKIA WASIOONA DAR NA PWANI
Na Mwandishi Wetu
WATU wasioona kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wamenufaika na mafunzo yaliyotolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa lengo la kuwawezesha kushiriki shughuli za uzalishaji kwa kuzingatia kanuni bora za usalama na afya kazini.
Mafunzo hayo ya siku moja ambayo yametolewa kwa wanachama 50 wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania (TAB) yamehusisha mada mbalimbali zikiwemo utambuzi na udhibiti wa vihatarishi vya usalama na afya pamoja na misingi ya huduma ya kwanza mahali pa kazi.
Washiriki wa mafunzo hayo wanajihusisha na shughuli mbalimbali zikiwemo ushonaji, kilimo, ufugaji, uzalishaji wa bidhaa zikiwemo sabuni na biashara ndogondogo.
Akifunga mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema Taasisi anayoiongoza inatambua thamani na mchango wa watu wenye ulemavu katika kujenga uchumi wa Taifa jambo ambalo limepelekea mafunzo hayo kuandaliwa pamoja na mafunzo mengine ambayo OSHA imekuwa ikayatoa kwa makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu.
“Niwapongeze washiriki wote wa mafunzo kwa kuitikia mwaliko wa kushiriki mafunzo haya muhimu kwenu kwani ni dhahiri kuwa ulemavu ni hali tu ambayo haipaswi kuwa kikwazo kwenu kushiriki katika shughuli za kiuchumi,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA na kuongeza:
“Sambamba na mafunzo haya, tutawapatia vifaa saidizi zikiwemo fimbo nyeupe, karatasi za nukta nundu pamoja na vitabu maalum vya nukta nundu vyenye maudhui ya mafunzo ya usalama na afya kwa ajili ya rejea zaidi.”
Aidha, Mwenda ameahidi kuwa mafunzo ya usalama na afya kwa makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu yatafuatiwa na zoezi la kutembelea maeneo yao ya kazi kwa ajili ya kutathmini mazingira ya kazi ili kushauri namna sahihi ya kuboresha mazingira hayo.
Awali, akiwasilisha salamu za Jumuiya ya Wasiiona Tanzania, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Omary Itambu, ameipongeza OSHA kwakuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha watu wasioona pamoja na makundi mengine ya watu wenye ulemavu.
“Tunaiomba OSHA kuendeleza utamaduni huu wa kutujali watu wenye ulemavu," ameeleza Bw. Itambu.

Comments
Post a Comment