DC MPOGOLO ATOA WITO KWA MADIWANI, WENYEVITI KUSHIRIKIANA NA TANESCO
Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa kutoka Halmashauri za Manispaa za Ilala, Temeke na Kigamboni kushirikiana kikamilifu na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ikiwemo kulinda miundombinu ya umeme na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya huduma hiyo.
Mpogolo alitoa wito huo jijini Dar es Salaam leo, Novemba 20, 2025, wakati akifungua kikao kazi kilichoandaliwa na Tanesco kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, lengo likiwa kuimarisha ushirikiano baina ya shirika hilo na viongozi wa serikali za mitaa ili kuboresha upatikanaji wa huduma za umeme.
Amesema viongozi wa mitaa na madiwani ni kiungo muhimu kati ya serikali na wananchi, hivyo kupitia mafunzo hayo kutawasaidia kutatua changamoto za wananchi kwa uharaka na ufanisi zaidi.
“Kupitia viongozi hawa tunapata taarifa zote muhimu kutoka kwenye jamii. Nawapongeza kwa kuwa hawa ni viongozi wanaochaguliwa na wananchi, hivyo mafunzo haya yataongeza uelewa wao katika kushughulikia changamoto za umeme,” alisema.
Mpogolo amelipongeza Shirika la Tanesco kwa kuandaa mafunzo hayo na kuonesha mwelekeo mpya wa kuboresha huduma, akisema kikao kazi hicho kinatoa taswira ya kazi zinazotekelezwa na shirika hilo pamoja na mikakati ya kuongeza ufanisi na kuimarisha mawasiliano na wananchi.
Aidha, amesifu hatua ya Tanesco kuanzisha mfumo wa i-Konnect na namba maalum ya huduma 180, vilivyolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma bila wananchi kulazimika kufika ofisini.
Amepongeza pia maboresho ya mifumo ya mawasiliano ambayo imesaidia kuongeza uwazi na upatikanaji wa taarifa kwa wakati.
“Niwahakikishie Tanesco kwamba kupitia mnavyofanya leo, mtaongeza ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi. Endeleeni kutoa elimu na kushirikiana kwa karibu na watendaji wa wilaya ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma,” amesema
Kwa upande wake, Kaimu Mkurungezi wa Mawasiliano na Uhusiano wa umma Tanesco, Irene Gowelle, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa shirika huo wa kukuza ushirikiano na wadau wake, hususan viongozi wa kata na mitaa wanaofanya kazi kwa ukaribu na wananchi.
Amesema kikao kazi hicho kimeandaliwa ili kutoa taarifa kuhusu miradi mbalimbali ya umeme, kuimarisha mawasiliano na kuwaelimisha viongozi hao juu ya matumizi ya majiko ya umeme na umuhimu wa kulinda miundombinu ya shirika hilo.
“Tanesco inatambua nafasi ya viongozi wa mitaa katika kuhakikisha wananchi wanahudumiwa vizuri. Leo tutatoa mawasilisho kuhusu miradi ya umeme, umuhimu wa miundombinu ya shirika na maboresho tunayoyaendelea kufanya,” amesema Gowelle.
Ameongeza kuwa Tanesco imejidhatiti kuboresha huduma kwa kuimarisha mifumo ya mawasiliano, kuongeza njia mbadala za kupata huduma na kuwezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi zaidi kupitia teknolojia.


Comments
Post a Comment