DIWANI RYOBA MREMA AJITOSA KUWANIA UNAIBU MEYA WA JIJI LA DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
DIWANI wa Kata ya Kinyerezi, Manispaa ya Ilala, John Ryoba Mrema (maarufu kama Wahenga), amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa katika kiti cha unaibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam .
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu, mapema leo Novemba 21,2025 katika Ofisi za CCM Wilaya ya Ilala,Diwani Ryoba alisema hatua yake ya kuwania nafasi hiyo inalenga kuimarisha umoja wa madiwani na kuongeza ushirikiano kati ya serikali za mitaa na Serikali Kuu, hususan katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“Kwanza nawashukuru wananchi wa Kinyerezi kwa kuniamini na kunichagua kwa kura nyingi kuwa diwani wao. Pia nampongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushindi mkubwa alioupata na kwa kuunda Serikali thabiti chini ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba na Makamu wa Rais Dkt. Emmanuel Nchimbi,” alisema.
Ryoba amebainisha kuwa dhamira yake ni kuhakikisha Halmashauri ya Jiji inakuwa na uongozi wenye mshikamano na uwajibikaji, huku akimsaidia Meya atakayechaguliwa kuongoza vikao na kufuatilia utekelezaji wa maamuzi kwa manufaa ya wananchi.
“Nimejitokeza kuwania nafasi ya Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kipindi cha 2025/2030. Lengo langu ni kuwaunganisha madiwani na kuhakikisha wananchi wanapata majibu ya matarajio yao,” alisisitiza.
Aidha, amesema amejiandaa kutoa ushirikiano wa karibu kwa Serikali Kuu, Mkuu wa Mkoa na Mkurugenzi wa Halmashauri ili kuhakikisha Ilala inapiga hatua kubwa za maendeleo katika miaka mitano ijayo.


Comments
Post a Comment