WAZIRI KAPINGA -FCC NI NGUZO MUHIMU YA KULINDA WALAJI NA KUDHIBITI BIDHAA BANDIA.

 




Na Mwandishi wetu

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt. Judith Kapinga, amesema Tume ya Ushindani (FCC) ina mchango mkubwa katika mustakabali wa taifa hususan katika kulinda maslahi ya walaji na kudhibiti bidhaa bandia sokoni.

Akizungumza leo Novemba 24, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake katika tume hiyo, Dkt. Kapinga amesema  lengo la ziara hiyo ni kuzungumza na watendaji wa FCC ili kuimarisha misingi ya utekelezaji wa majukumu ya wizara yake.

Amesema FCC imekuwa ikifanya kazi zake kwa ufanisi na mchango wake unaonekana katika jamii, hususan katika kudhibiti bidhaa zisizo na ubora na kusimamia ushindani wenye tija.


“Ziara yangu imelenga kuimarisha misingi iliyowekwa ili kuongeza ubora na ufanisi, kwani Watanzania wanaitegemea Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia taasisi zake za udhibiti na uratibu, ikiwemo FCC ambayo imekuwa ikiboresha utendaji kazi ili kufikia mategemeo ya walaji,” amesema 

Aidha amesema kupitia kikao hicho wameweka mikakati mizuri ya kuboresha ufanisi pamoja na kuongeza ubunifu, ikiwemo kushirikiana na sekta binafsi katika kutekeleza majukumu yetu,” 

Pamoja na hayo, Dkt. Kapinga amesema  wizara yake itaendelea kuimarisha na kuongeza kongani za viwanda nchini, kwa kuwa viwanda vinachochea ajira, kuongeza mapato ya ndani na nje, na kuimarisha uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema  tume hiyo iko katika hatua za mwisho za kuandaa Baraza la Kitaifa la Utetezi wa Walaji, ambalo litatoa jukwaa kwa wananchi kushiriki moja kwa moja katika kulinda na kusimamia haki zao za kibiashara.




Amesema  baraza hilo litakuwa na jukumu la kufuatilia mwenendo wa masoko, kushughulikia malalamiko ya walaji kwa wakati na kuhakikisha mazingira ya biashara yanabaki kuwa ya haki na yenye uadilifu.

Ngasongwa ameongeza kuwa uanzishwaji wa baraza hilo ni sehemu ya juhudi endelevu za FCC katika kuimarisha nidhamu ya ushindani na ulinzi wa walaji kwa kuhakikisha masoko yanafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Comments

Popular posts from this blog

WANAFUNZI WALIOMALIZA KIDIA SEKONDARI WACHANGIA UJENZI WA KANISA SH MILLION 20

VETA YAJIPANGA KUSHIRIKINA NA TOYOTA TANZANIA KUIMARISHA MAFUNZO YA UFUNDI MAGARI

UJENZI WA BWAWA LA KUFUA UMEME LA MTO MALAGARASI , WAPIGA HATUA MPYA