WAZIRI NDEJEMBI AHIMIZA WANANCHI KULINDA MIUNDOMBINU YA UMEME
Asisitiza utunzaji wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji.
Asisitiza pia ulinzi na usalama wa miundombinu ya umeme.
Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi amewahimiza wananchi kuhakikisha ni jukumu la kila mwananchi kushiriki katika kuitunza na kuilinda miundombinu ya umeme, ili kuepusha hasara kwa serikali na usumbufu wa huduma muhimu zinazotumia nishati ya umeme.
Waziri Ndejembi amebainisha hayo Novemba 26,2025 wakati wa ziara yake ya kwanza ya kutembelea mradi wa bwawa la kufua umeme wa Julius Nyerere-JNHPP wa megawati 2115 Mkoani Pwani, kwa lengo la kuona maendeleo ya mradi huo.
Akiwa katika ziara hiyo Mhe. Ndejembi amesisitiza pia utunzaji wa mazingira na kuhifadhi vyanzo vya maji, ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa muda mrefu.
“ Serikali imewekeza fedha nyingi takribani Shilingi trilioni 6.558 ili kuhakikisha watanzania wanapata umeme wa kutosha na wa uhakika wakati wote, hivyo tuone namna gani bora ya kulinda vyanzo vyetu tukishirikiana na TFS pamoja na TAWA, sambamba na kushirikiana na wizara nyingine kama Kilimo, maji pamoja na mifugo “ Alisema Ndejembi.
Aliongeza kuwa kwa kufaya hivyo tutaweza kuboresha na kutunza miundombinu hiyo bila kuathiriwa na shughuli za kibinadamu kwenye mradi huu, na kutunza vyanzo vya maji ili mradi uweze kudumu na kuendelea kupata umeme wa uhakika.
Aidha Ndejembi amesisitiza suala zima la ulinzi na usalama kwa kuongeze nguvu katika ulinzi wa miundombinu ya mradi wa JNHPP, huku akitoa wito kwa wakandarasi pamoja na viongozi kujenga utaratibu imara wa ufuatiliaji kwa kuwa mradi huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa umeme wa uhakika kwa kiwango kikubwa, hivyo kuimarisha uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania( TANESCO) Lazaro Twange ameeleza kuwa mitambo ya uzalishaji umeme JHNPP imekamilika na imeanza kuzalisha megawati 950 ambazo zinatosheleza mahitaji yaliyopo na hivyo kupunguza Mgao wa umeme huku akieleza kuwa shirika linaendelea kujenga njia za kusambaza umeme ili kupeleka umeme wa uhakika kwa wananchi.
“Baada ya kukamilika kwa asilimia 100 ya ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), Serikali imehamishia nguvu kubwa katika ujenzi wa njia za kusafirisha umeme ili kuunganisha mikoa mbalimbali nchini”. Amehimiza Bw. Twange
Katika ziara hiyo Ndejembi ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Dkt. James Mataragio, pamoja na Wataalamu wengine wa wizara ya Nishati.




Comments
Post a Comment