MBUNGE SHINGO KUSAIDIA VIJANA UKONGA MAFUNZO YA UDEREVA
Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Jimbo la Ukonga, Bakari Shingo amesema yupo tayari kuwasaidia vijana wa jimbo hilo kwa kuwapatia mafunzo ya udereva wa bajaji na bodaboda, lengo likiwa kuwawezesha kupata ajira na kujikwamua kiuchumi.
Shingo ameyabainisha hayo jijini Dar es Salaam katika kikao cha Baraza la Madiwani kilicholenga kumchagua Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Shingo amesema mafunzo hayo yameanza Desemba 3, 2025 na tayari vijana zaidi ya 140 wameanza mafunzo hayo ya awamu ya kwanza.
Amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa gharama za Mbunge na Mfuko wa Mbunge, yakilenga vijana wote wa Jimbo la Ukonga ambao hawana leseni au ujuzi wa udereva.
“Tunahakikisha vijana wasiokuwa na leseni wanapata leseni, na wasiojua kabisa kuendesha wanapatiwa mafunzo. Lengo langu ni kuwafikia vijana kati ya 600 hadi 800,” amesema Shingo.
Aidha, Mbunge huyo ameahidi kushirikiana kwa karibu na Baraza la Madiwani pamoja na Mstahiki Meya mpya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilali Juma, katika kuleta maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.
Katika kikao hicho, Mstahiki Meya Nurdin Bilali alichaguliwa kwa kura 48 za ndiyo kati ya kura 51 zilizopigwa, huku Naibu Meya, John Mrema, akipata kura 49 za ndiyo katika uchaguzi uliohusisha vyama vya CCM, Chauma na ACT-Wazalendo.
Mbunge Shingo alimpongeza Meya mpya kwa ushindi huo na kuahidi ushirikiano wenye tija kwa maendeleo ya jiji na ustawi wa wananchi.

Comments
Post a Comment