WATANZANIA WAHIMIZWA KUILINDA AMANI NA KUTOKUKUBALI KUGAWANYWA
Na Mwandishi wetu
WATANZANIA wametakiwa kuendelea kulinda na kudumisha amani, umoja na utawala wa sheria kwa kukataa vikali vitendo, kauli au mikakati inayolenga kuingiza nchi kwenye machafuko, vurugu au migawanyiko ya kisiasa.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam mapema leo Desemba 23,2025 na Aliyekuwa mgombea wa Bavicha Taifa, Masoud Mambo, wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo alisema kuwa demokrasia ya kweli hujengwa kwa hoja, heshima ya sheria na ushindani wa sera, si kwa mashinikizo wala siasa za misimamo mikali.
Mambo amesema Watanzania wanapaswa kuiunga mkono Serikali iliyopo madarakani katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa maslahi ya Taifa, akisisitiza kuwa Serikali hujengwa na kuimarishwa na wananchi wake kupitia mshikamano na uwajibikaji.
"Tanzania ni mali ya Watanzania wote na kwamba amani si zawadi bali ni jukumu la kila mmoja. “Umoja wetu ndiyo nguvu yetu,” amesisitiza Mambo, huku akiwataka wananchi kuilinda amani ya nchi kwa wivu mkubwa"amesema
Aidha, ameeleza kuwa Tanzania ni nchi inayotawaliwa na sheria, na kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, vyama vyote vilivyosajiliwa kisheria ni sawa mbele ya sheria bila ubaguzi wowote.
Amesema jaribio lolote la kubeza, kudharau au kupuuza ushiriki wa vyama fulani vya siasa katika chaguzi, mijadala au majukwaa ya kitaifa kwa kigezo cha vyama vingine kususia, ni kinyume cha misingi ya demokrasia, haki na usawa.
Amesisitiza kuwa kila chama cha siasa kina haki ya kushiriki au kutoshiriki katika mchakato wowote wa kisiasa, lakini haki hiyo haiwezi kutumika kama chombo cha kulazimisha nchi kuyumba au kuvuruga utulivu wa Taifa.
Kwa mujibu wa Mambo, lengo la vyama vya siasa ni kushika dola ili kutekeleza sera zao kwa maendeleo ya nchi na wananchi, jambo ambalo haliwezi kufikiwa katika mazingira ya machafuko, chuki, uhasama na migawanyiko ya kisiasa.
Aidha, amewakumbusha Watanzania kuwa changamoto za kisiasa hazitatuliwi kwa maandamano yanayovunja amani, lugha za uchochezi wala kampeni za kuichafua nchi ndani na nje ya mipaka yake.
Amesema njia sahihi na ya kizalendo ya kushughulikia changamoto hizo ni kutumia meza ya mazungumzo, majadiliano ya wazi yenye hoja, mifumo ya kisheria iliyopo pamoja na elimu ya uraia ili wananchi waweze kupima masuala mbalimbali na kufanya maamuzi kwa busara.

Comments
Post a Comment