KIBANZI CHA SERIKALI, BORITI YA KANISA: MGOGORO WA MAADILI KATIKA UONGOZI WA DINI
TAFAKURI YA JUMAMOSI
Kanisa linapojipa uhuru wa kuikosoa Serikali, linawajibika pia kusikiliza na kuvumilia sauti za waumini wake vinginevyo haki hugeuka kuwa unafiki.
Na. Godwin Jickson, Muumini Kanisa Katoliki
Tafakuri ya dhamiri ya Kanisa
Tafakuri ya Jumamosi hii inalenga zaidi dhamiri ya Kanisa kuliko mjadala wa kisiasa.
Inalenga mtazamo wa haki, si upande wa chama; maadili ya kichungaji, si shambulio la mtu; na uthabiti wa Injili, si kelele za mitandao.
Kwa kipindi kirefu sasa, Kanisa Katoliki nchini limejikuta katikati ya mjadala mkali unaohusu uhuru wa kujieleza, haki ya kukosoa, na mipaka ya mamlaka ya kichungaji.
Mjadala huu umechochewa na majibu makali ya baadhi ya viongozi wa Kanisa dhidi ya waumini waliotoa maoni mbadala au ukosoaji waliotaka Padri Charles Kitima ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu (TEC) kulitengenisha baraza hilo na kanisa kwa ujumla katika mahusiano na CHADEMA
Swali la msingi ni: Je, Kanisa linaweza kudai haki ya kuikosoa Serikali bila masharti, lakini likashindwa kuvumilia kukosolewa na waumini wake? Ikiwa jibu ni hapana, basi tunapaswa kukiri kwa unyenyekevu kwamba tumetumbukia katika unafiki wa haki hali ambayo Yesu aliionya waziwazi.*
Uhuru wa Kuhoji ni haki ya wote au ya wachache?
Kwa miaka mingi, viongozi wa Kanisa wamekuwa mstari wa mbele kusisitiza umuhimu wa uhuru wa kujieleza wanapokosoa Serikali, sera zake, au mwenendo wa kisiasa.
Hoja zao mara nyingi zimejengwa juu ya msingi wa haki za binadamu, maadili ya kijamii, na wajibu wa Kanisa kuwa *“sauti ya wasio na sauti”.
Huu ni msimamo unaokubalika kimaadili na kikanisa.
Lakini tatizo linajitokeza pale kanuni hiyo hiyo inapokataliwa inapotumika ndani ya Kanisa lenyewe.
Waumini wanapouliza maswali, kuonya, au kukosoa mwenendo wa viongozi wao, majibu yanayojitokeza si hoja za kitheolojia au kikanuni, bali kejeli, dharau na matusi.
Hapo ndipo haki inapopoteza uhalali wake.
Majibu yaliyogeuka kuwa dharau
Katika hotuba na kauli za hadhara, Askofu Mkuu Ruwa’ichi amenukuliwa akiwajibu wakosoaji kwa lugha kali na kejeli ikiwa ni pamoja na kuwaita “Malofa”, “wapumbavu,” “wajinga,” “Wasaliti”, “Njaa Njaa”. “wasio na akili,” au kuwadhalilisha kwa maneno yanayopunguza hadhi yao kama waumini.
Haya hayakuwa majibu ya hoja kwa hoja; yalikuwa matusi ya mamlaka dhidi ya hoja za waumini wanaolitakia heri kanisa lao .
Tafakuri ya kikanisa inatulazimisha kuuliza:
Je, lugha hii inaakisi roho ya Injili? Je, matusi na kejeli ni zana halali za kichungaji? Au ni ishara ya mamlaka yanayohofia kuulizwa maswali?
SHERIA YA KANISA (CANON LAWS ) INASEMAJE?
Sheria ya Kanisa Katoliki iko wazi kuhusu haki na wajibu wa waumini pamoja na mienendo inayotarajiwa kwa wachungaji wao:
*“•Canon 212 §3: Waumini wana haki, na wakati mwingine wajibu, wa kutoa maoni yao kwa wachungaji kuhusu mambo yanayohusu mema ya Kanisa kwa heshima, busara na ukweli”.*
Ifahamike kuwa haki hii si zawadi ya Askofu; ni haki ya kikanisa.
Aidha,
•Canon 220: Inakataza kudhuru heshima njema na sifa ya mtu. Lugha ya dharau, kejeli na matusi ni kinyume cha kifungu hiki.
Kadharika,
•Canon 384: Inamtaka Askofu awe mfano wa busara, kiasi na upendo wa kichungaji, akilinda umoja wa Kanisa.
Lugha kali inayogawa waumini inakiuka wajibu huu.
Kama ambavyo inaendelea zaidi
•Canon 1373 (kwa tahadhari): Inahusu kuchochea chuki au uasi dhidi ya mamlaka ya Kanisa.
Tafsiri sahihi inahitaji busara lakini ukosoaji wa heshima hauwezi kufasiriwa kama chuki.
Kwa msingi huu, hakuna Canon Law inayoruhusu matusi kama majibu.
Ukosoaji hujibiwa kwa hoja, si kwa kudhalilisha.
MKANGANYIKO WA KICHUNGAJI NA SIASA*
Chanzo kingine cha mvutano ni wasiwasi wa waumini kuhusu mwenendo wa Padri Charles Kitima.
Baadhi ya waumini wanaona kuwa kiongozi huyo anachanganya majukwaa ya Kanisa na misimamo binafsi ya kisiasa, akihusishwa wazi na mitazamo ya CHADEMA.
Iwe mtu anakubaliana na tathmini hii au la, jambo la msingi ni kuwa: *wasiwasi huo una haki ya kusikilizwa.
Kwa kuzingatia kuwa Kanisa, kiasili, ni mama na mwalimu hivyo linapochanganya ujumbe wa wokovu na ajenda za vyama, linafanya waumini wake wagawanyike, linapoteza hadhi ya upatanisho, na linaweka doa kwenye dhamira yake ya kiroho.
Hili ndilo tamanio la waumini si uasi, bali ulinzi wa Kanisa.
ISEMAVYO BIBLIA KUHUSU LUGHA ZA MAMLAKA*
Maandiko Matakatifu yanatoa mwanga usio na shaka katika rejea mbalimbali za ki biblia.
Mfano:-
•“Neno lenu na liwe daima na neema.” (Wakolosai 4:6)
•“Heri wapatanishi.” (Mathayo 5:9)
•“Msihukumu, msije mkahukumiwa.” (Mathayo 7:1)
•“Kifo na uzima viko katika ulimi.” (Mithali 18:21)
Lakini juu ya yote, Yesu anatupatia kioo cha kujitazama:*
“Kwa nini waona kibanzi kilicho katika jicho la nduguyo,
lakini huoni boriti iliyo katika jicho lako?” - Mathayo 7:3
UZITO WA TAFAKURI
Hapa ndipo tafakuri inakuwa nzito:
tunawezaje kudai haki ya kukosoa Serikali, lakini tukashindwa kuvumilia kukosolewa na waumini? Huu ni mgongano wa maadili unaohitaji toba ya pamoja, si majibu ya hasira.
NGUVU YA KANISA NI KUSIKILIZA
TAFAKURI hii inatueleza kuwa Kanisa lenye afya halihofii maswali, hoja wala mijadala inayoibuliwa sio tu na waumini hata jamii kwa ujumla
Historia ya Kanisa inaonyesha kuwa marekebisho (reforms) mengi yalianza kwa maswali magumu kutoka ndani.
Ifahamike wazi kuwa kusikiliza si udhaifu ni nguvu ya kichungaji
ieleweke wazi kuwa kukosolewa si kudharauliwa ni mwanga wa kujirekebisha.
Tafakuri inaona viongozi wanapojibu maswali kwa kejeli, wanatuma ujumbe hatari kwamba mamlaka hayawajibiki.
Hilo linazalisha hofu, ukimya wa kinafiki, na mgawanyiko yote ambayo ni kinyume cha Injili.
USHAURI WA KICHUNGAJI*
Je, Kanisa linapaswa kuwa vipi?
Ili kurejesha uaminifu na umoja, Kanisa linapaswa kufanya ifuatavyo:
1.Kujenga utamaduni wa kusikiliza
Kuanzisha majukwaa ya mazungumzo ya heshima kati ya viongozi na waumini.
2.Kurejesha lugha ya Injili, kujibu hoja kwa neema, si kwa matusi. kwa busara, si kwa kejeli.
3. Kutenganisha wazi Kanisa na siasa za vyama, Kanisa libaki sauti ya dhamiri ya taifa, si jukwaa la chama.
4. Kuheshimu Canon Law kwa vitendo kutambua haki ya waumini (Canon 212 §3) na kulinda heshima yao (Canon 220).
5. Kujitathmini kabla ya kujitetea
Kabla ya kushambulia wakosoaji, viongozi wajitazame kwanza.
Hitimisho: Haki isiyo na unyenyekevu hugeuka unafiki
Tafakuri ya Jumamosi hii inatualika sote viongozi na waumini kurudi kwenye unyenyekevu wa Injili.
Haki ya kuikosoa Serikali ni halali; lakini haki hiyo hiyo lazima iheshimiwe ndani ya Kanisa.
Vinginevyo haki hugeuka kuwa silaha ya upande mmoja.
Kanisa ni la Kristo, si la mtu.
Kanisa ni waumini.
Na ukweli, kama Injili inavyotufundisha, hauogopi maswali.

Comments
Post a Comment