TANZANIA YASISITIZA UONGEZAJI THAMANI MADINI BARANI AFRIKA
Tanzania yajipanga kuwa kitovu cha uongezaji thamani madini Afrika.
Yashauri kuhusu ushirikiano wa kikanda na kisekta.
Riyadh, Saudi Arabia
TANZANIA imetambua shughuli za uongezaji thamani madini kama nguzo muhimu ya kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii lengo kubwa ikiwa ni kuondokana na uuzaji na usafirishaji wa madini ghafi kwa nchi zinazozalisha madini mbalimbali Barani Afrika.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa, wakati akizungumza kwenye Kongamano la Kimataifa la Madini lijukanalo kama Future Minerals Forum 2026 lililowakutanisha mawaziri, viongozi mashuhuri na wadau wa sekta ya madini kutoka zaidi ya nchi 100 ndani na nje ya Bara la Afrika.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa, rasilimali madini ni moja ya utajiri mkubwa uliopo Barani Afrika hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuweka mkazo katika shughuli za uongezaji thamani madini ndani ya nchi za Afrika ambapo kama kila nchi itazingatia hilo itakuwa moja ya ufunguo wa kubadilisha utajiri wa madini kuwa kichocheo cha maendeleo endelevu kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Akielezea kuhusu juhudi mbalimbali zinafanywa na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza Sekta ya Madini, Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha miundombinu ya usafirishaji na mawasiliano ikiwemo ujenzi wa reli ya mwendo kasi, barabara, nishati ya umeme na uongezaji wa bandari ili kuhakiskisha rasilimali zinasafirishwa kwa urahisi kutokea mgodini na kiwandani.
Dkt. Kiruswa amefafanua kuwa, ili kufanikisha hilo ni vyema kila taifa liendeleze viwanda vya uchakataji, uchenjuaji na usafishaji madini akitolea mfano kwa taifa la Tanzania linavyoendeleza juhudi mbalimbali katika mnyororo wa thamani madini ikiwemo kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, mifumo ya usafirishaji katika ngazi ya kimataifa kupitia Bandari ya Dar es Salaam.


Comments
Post a Comment