UJUMBE NA MAFUNDISHO YA KARDINALI ARINZE NA HESHIMA YA MISA TAKATIFU
- Get link
- X
- Other Apps
UJUMBE na mafundisho ya Cardinal Francis Arinze, aliyewahi kuongoza Idara ya Ibada ya Kimungu Vatican, yanaendelea kutajwa kama rejea muhimu kuhusu nafasi na heshima ya Misa Takatifu ndani ya Kanisa Katoliki.
Arinze amekuwa akisisitiza kuwa Misa ni ibada ya kumuabudu Mungu, kuomba msamaha, kushukuru na kutafuta neema, na si jukwaa la burudani, mijadala au hisia binafsi.
Katika siku za hivi karibuni, mijadala imeibuka miongoni mwa waumini kuhusu maudhui na mitindo ya baadhi ya mahubiri, hali iliyoibua tafakuri pana juu ya mpaka uliopo kati ya maonyo ya kichungaji na lugha inayoweza kutafsiriwa tofauti na wasikilizaji.
Wachambuzi wa masuala ya imani wanasema mijadala hiyo inaonyesha hitaji la pande zote kusikilizana kwa unyenyekevu na hekima ya kichungaji.
Mafundisho ya Kanisa, yakisaidiwa na Maandiko Matakatifu, yanahimiza lugha ya upole, heshima na kujitathmini, hususan katika maeneo matakatifu.
Biblia inaonya dhidi ya dharau na maneno makali mbele ya Mungu, ikisisitiza kwamba madhabahu ni mahali pa uponyaji wa roho na kuimarisha umoja wa waumini.
Kwa mujibu wa wataalamu wa teolojia, changamoto zinazojitokeza ndani ya jumuiya ya waumini si jambo geni katika historia ya Kanisa, bali ni sehemu ya safari ya imani inayohitaji busara, mazungumzo ya ndani na uongozi unaojengwa juu ya unyenyekevu. Wanasema kukosoa kwa heshima na kujitathmini kwa viongozi na waumini ni sehemu ya utamaduni wa Kanisa unaolenga kujenga, si kubomoa.
Viongozi wa dini duniani, akiwemo Papa Francis, wamewahi kukumbusha kuwa madhabahu na mimbari ni mahali pa kuunganisha, kuponya na kuimarisha matumaini, si mahali pa kuendeleza migawanyiko au ajenda zinazoweza kuwagawa waumini. Msisitizo huu unaonekana kufanana na onyo la Cardinal Arinze kuhusu hatari ya ibada kupoteza mwelekeo wake wa kiroho.
Kwa mtazamo huo, tafakuri hii inaonekana kuwa mwaliko wa kurejea katika misingi ya ibada yenye heshima, utulivu na upendo, huku Kanisa likiendelea kutekeleza wajibu wake wa kuwa mama na mwalimu wa waumini wote. Lengo kuu linabaki kuwa kulinda utakatifu wa Misa na kudumisha umoja wa Kanisa katika nyakati zenye mijadala na mitazamo tofauti.
- Get link
- X
- Other Apps

Comments
Post a Comment