VIJANA DAR WAUNGANA KUMUONESHA UPENDO RAIS DKT. SAMIA KATIKA SIKU YAKE YA KUZALIWA
Na Mwandishi wetu
VIJANA na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam leo wameungana kumuonesha upendo na heshima Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake Januari 27, wakieleza kuridhishwa na uongozi wake unaowekeza na kuzalisha fursa kwa vijana.
Akizugumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya bora Jijini Dar es salaam Januari 27,2026 Mratibu wa Taasisi ya Together For Samia, Gulatone Masiga, ambaye ni mmoja wa waandaaji wa hafla hiyo, amesema lengo la mkusanyiko huo ni kuwakutanisha vijana wa kizazi kipya pamoja na wananchi wenye mapenzi mema kwa Taifa ili kumuonesha Rais heshima na shukrani.
Masiga amesema Rais Dkt. Samia ni kiongozi anayefungua milango ya fursa kwa vijana, mlezi wa ndoto zao na anayesikiliza mawazo ya kizazi kipya huku akisimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa usawa kote nchini.
“Hii si sherehe tu, bali ni ishara kwamba vijana wa kizazi kipya na wananchi wenye mapenzi mema kwa Taifa tunatambua uongozi unaotujali na kutupa nafasi. Tumeona ni vyema kuandaa shughuli ya kuwakutanisha ili kuonesha upendo na heshima kwa Rais ambaye ni mlezi wa vijana na maendeleo ya Taifa,” amesema Masiga.
Amesema vijana walioshiriki katika hafla hiyo ni wa kizazi kipya ambao wamenufaika kwa kiasi kikubwa na uongozi wa Rais Dkt. Samia katika takribani miaka mitano ya uongozi wake.
Akieleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, Masiga alitaja ujenzi wa vyuo vya ufundi na ujuzi katika wilaya zaidi ya 62 nchini, hatua iliyowezesha vijana wengi kupata maarifa na stadi za kujiajiri.
Pia amesema Serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kuanzisha mtaala mpya unaolenga kuhakikisha wahitimu wa elimu ya msingi na sekondari wanapata maarifa na vyeti vinavyowawezesha kujiajiri.
“Tumeona hatuna sababu ya kutofurahia siku ya leo na kuonesha upendo wetu kwake,” alisema, akisisitiza kuwa uongozi wa Rais umehakikisha maendeleo yanafika kila kona ya nchi.
Kwa upande wake, kijana mzalendo Dorcas Mshiu amesa anasimama kifua mbele kusherehekea siku hiyo maalumu ya Rais Dkt. Samia, akieleza kuwa Rais huyo amekuwa mama anayewakumbuka vijana na kuwafungulia fursa mbalimbali.
Amesema kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, vijana wengi wameanza kusajili biashara zao, hali inayoonesha kuwa mazingira ya biashara yamefunguka.
"Rais Dkt. Samia amefungua milango ya uwekezaji, hali iliyoongeza ajira kwa vijana wengi nchini... vijana wanaojiajiri wamenufaika na mkakati maalumu wa mikopo yenye riba ya asilimia nne, unaowawezesha kuanzisha na kuendeleza biashara zao hivyo Mama yetu asituache sisi kama GEZ; tunasema mama ni mlezi wa GEZ,” amesema Dorcas.












Comments
Post a Comment