ZOEZI LA NIDA BUYUNI LAFANIKIWA, WANANCHI WAPONGEZA
Na Mwandishi wetu
WANANCHI wa Kata ya Buyuni, jijini Dar es Salaam, wameipongeza Serikali kwa kuwasogezea karibu zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa (NIDA), wakisema hatua hiyo imepunguza usumbufu na gharama walizokuwa wakikabiliana nazo awali kufuata huduma hiyo mbali na makazi yao.
Wakizungumza leo Januari 30, 2026 jijini Dar es Salaam, katika kilele cha zoezi hilo lililozinduliwa rasmi Januari 19, 2026, wananchi hao wamesema uandikishaji huo umewasaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa ambavyo ni muhimu kwa huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Buyuni, Jamalidin Amri amesema zoezi la uandikishaji limekwenda vizuri na kufanikiwa kutokana na usimamizi mzuri wa viongozi wa kata pamoja na ushirikiano uliotolewa na Serikali, huku akiomba zoezi hilo liendelee ili kuwafikia wananchi wengi zaidi wanaohitaji huduma hiyo.
"Mahitaji ya vitambulisho vya Taifa bado ni makubwa kwa wananchi, hivyo tunaiomba Serikali zoezi hili kuwa endelevu ili kusaidia kupunguza changamoto kwa wananchi wanaokosa huduma mbalimbali zinazohitaji kitambulisho cha NIDA"amesema
Kwa upande wake, Salama Kumbi, mkazi wa Chanika katika Kata ya Buyuni, amesema zoezi hilo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa na kuwasaidia wananchi waliokuwa na changamoto kwa muda mrefu, akisema yeye binafsi ameweza kukamilisha usajili wake baada ya kukwama hapo awali.
Naye Rehema Jabir Kibiri amesema licha ya changamoto ya wingi wa wananchi na foleni ndefu, wananchi wengi wamefanikiwa kupata huduma hiyo, huku akimpongeza Diwani wa Kata ya Buyuni, Jesca Msolla, kwa jitihada zake za kuwasogezea wananchi huduma za NIDA karibu na maeneo yao.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Diwani wa Kata ya Buyuni, Jesca Msolla, amesema uandikishaji huo umehitimishwa kwa mafanikio baada ya zaidi ya wananchi 2,000 kujitokeza kujiandikisha, huku akitoa wito kwa wananchi kufuata maelekezo ya Serikali ya kata na kuepuka madalali vishoka wanaowadanganya wananchi kuhusu huduma za NIDA.








Comments
Post a Comment