ETDCO YAAHIDI KUKAMILISHA MRADI WA UMEME KATIKA VITONGOJI 372 RUVUMA KWA WAKATI
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Ahmed (kushoto), akikabidhiwa nakala ya mkataba na Meneja wa Usimamizi wa Miradi ya Kusambaza Umeme wa REA, Mhandisi Deogratius Nagu, katika hafla ya makabidhiano ya utekelezaji wa mradi kati ya ETDCO na REA, iliyofanyika Januari 3, 2026 Mkoani Ruvuma.
Na Mwandishi wetu
KAMPUNI ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) imeahidi kukamilisha kwa wakati mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 372 wenye thamani ya shilingi bilioni 37.9, Mkoani Ruvuma.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya utekelezaji wa mradi huo kati ya ETDCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), iliyofanyika Januari 3, 2026 Mkoani Ruvuma, Mkuu wa Mkoa huo, Brigedia Jenerali Ahmed Ahmed, ameitaka Kampuni ya ETDCO kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati katika wilaya za Mbinga na Nyasa.
Brigedia Jenerali Ahmed, amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutachochea shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Mkoa huo, huku akiwahimiza wananchi kujiandaa kuweka miundombinu ya umeme majumbani (wiring) ili waweze kuunganishwa na huduma hiyo mara baada ya mradi kukamilika.
“Ujio wa umeme huo utasaidia kukuza shughuli za kiuchumi na biashara katika maeneo husika,” amesema Kanali Ahmed.
Meneja Usamamizi wa Miradi ya Kusambaza Umeme REA, Mhandisi Deogratius Nagu, amesema kuwa mradi huo unatarajiwa kuwanufaisha wateja takribani 11,914 katika Wilaya za Mbinga na Nyasa.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Mhandisi Richard Mwanja, ameishukuru Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuipa ETDCO fursa ya kutekeleza mradi huo, huku akieleza kuwa Kampuni hiyo imejipanga kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa
Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Mhandisi Richard Mwanja, akiahidi utekelezaji wa mradi kwa wakati na kwa kuzingatia viwango, mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mheshimiwa Brigedia Jenerali Ahmed Ahmed.
Kwa upande wao, Wananchi wa Mkoa wa Ruvuma wameipongeza Serikali kupitia REA kwa kuwaletea miradi ya kusambaza umeme katika vitongoji vyao, wakisema kuwa miradi hiyo itasaidia kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.





Comments
Post a Comment