MBUNGE WA KIGOMA MJINI AREJEA SHULE, AWAHAMASISHA WANANCHI KUCHAGAMKIA FURSA YA ELIMU
- Get link
- X
- Other Apps
Na Mwandishi wetu.
MBUNGE wa Kigoma Mjini amerejea rasmi shule kwa mara ya kwanza baada ya miaka kadhaa nje ya mfumo wa elimu, akichagua kusoma katika Shule ya Brothers Academy, huku akitoa wito kwa wananchi na wasanii kuchangamkia fursa ya kujiendeleza kielimu.
Akizungumza kuhusu uamuzi wake huo, Jijini Dar es salaam mapema leo Februari 11,2026 amesema kutokusoma si ugonjwa, lakini kunaweza kumnyima mtu fursa nyingi muhimu maishani.
Amesema kuwa sababu iliyomfanya ashindwe kuendelea na masomo awali ni kufariki kwa wazazi wake, jambo lililomlazimu kuanza kujitafutia maisha mapema.
"Baada ya kufiwa na mzazi wake, alianza kazi ya kutengeneza magari, baadaye akajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kisha kujikita katika muziki"amesema
Amesema kuwa Mwaka 2015 alishinda nafasi ya udiwani, mwaka 2020 akajihusisha na masuala ya redio na hatimaye kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini.
Mbunge huyo amesema ameamua kurejea shule ili kuongeza ujuzi na maarifa yatakayomwezesha kuwatumikia wananchi wa Kigoma Mjini kwa ufanisi zaidi katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
“Kama umepata fursa ya kusoma, soma kijana. Unaweza kuwa na kipaji, lakini bila elimu ni vigumu kufika mbali,” amesisisitiza.
Aidha, alitoa wito kwa wasanii na wananchi wote waliokosa fursa ya kuendelea na masomo kutokata tamaa, bali kujiunga na programu maalum za VIP zinazotolewa na Brothers Academy, ambazo zinamuwezesha mwanafunzi kusoma popote alipo kutokana na majukumu yake.
Amesema anaunga mkono juhudi za Rais katika kuwekeza zaidi kwenye sekta ya elimu na kwamba huu ni wakati sahihi kwa watu wazima na vijana waliokwama kimasomo kurejea darasani. Pia aliwashukuru wabunge wenzake kwa kuchangamkia fursa hiyo ya kujiendeleza kielimu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Brothers Academy, Robert Rwezaula ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi, amesema shule hiyo imesajiliwa chini ya Serikali kupitia mfumo wa elimu ya watu wazima na inalenga kutoa elimu ya sekondari kwa njia huria kwa wale ambao hawakupata nafasi ya kumaliza masomo yao.
Amesema programu zao zinamwezesha mwanafunzi kukamilisha elimu ya sekondari ndani ya miaka miwili, huku kidato cha sita kikisomwa kwa mwaka mmoja kwa lengo la kupata angalau alama tatu za ufaulu (credits).
Pia wanatoa masomo kwa wanafunzi waliofeli kidato cha nne na cha sita pamoja na darasa maalum kwa walioishia kidato cha nne.
Mbali na masomo ya kawaida, taasisi hiyo pia inatoa mafunzo ya kompyuta na ina kampasi mbili zilizopo Ukonga na Mbagala, pamoja na programu ya VIP inayomwezesha mwanafunzi kuhudumiwa popote alipo.
Amesema lengo lao ni kuwafikia vijana na watu wazima waliokosa fursa ya kusoma ili kuwapatia nafasi ya pili ya kutimiza ndoto zao za kielimu na kitaaluma.
#brotheracademy
- Get link
- X
- Other Apps

Comments
Post a Comment