WANANCHI KIVULE WAHIMIZWA KUJISAJILI NIDA
Na Mwandishi Wetu
WANANCHI wa Jimbo la Kivule, Kata ya Kivule, jijini Dar es Salaam, wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili waweze kutambulika rasmi na kunufaika na huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Wito huo umetolewa mapema leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo lililofanyika katika Kata ya Kivule, ambapo kilele cha zoezi kinatarajiwa kufikiwa Februari 13, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari, Diwani wa Kata ya Kivule, Rajabu Manyinya, amesema zoezi hilo linatarajiwa kudumu kwa siku 11 hivyo ni muhimu wananchi kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaendelea kutekeleza ahadi zake za kuwaletea tabasamu wananchi kwa kuwasogezea huduma muhimu karibu na maeneo yao, ikiwemo huduma ya vitambulisho vya Taifa.
“Namshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kutekeleza ahadi zake za kuwasogezea wananchi huduma muhimu kama NIDA,” amesema Manyinya.
Ameeleza kuwa zoezi hilo lina manufaa makubwa kwa wananchi, ikiwemo kupunguza gharama na usumbufu wa kusafiri hadi Makao Makuu ya NIDA katika Halmashauri ya Jiji la Ilala, yaliyopo Mombasa, kufuatilia vitambulisho hivyo.
Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Kivule wameipongeza Ofisi ya Diwani kwa kuratibu zoezi hilo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Idara ya Uhamiaji pamoja na wanasheria wanaosaidia upatikanaji wa viapo kwa wananchi wasio na vyeti vya kuzaliwa.
Mkazi wa Mtaa wa Kerezange, Rahma Mohamed Ali, amesema zoezi hilo limewarahisishia wananchi kupata kitambulisho cha Taifa ikilinganishwa na hapo awali walipolazimika kusafiri umbali mrefu hadi makao makuu ya NIDA.
“Namshukuru sana Diwani wetu pamoja na Rais Dkt. Samia kwa kutujali na kutuletea huduma hii karibu. Tunaomba zoezi hili liwe endelevu ili wananchi wengi zaidi wanufaike,” amesema Rahma.
Naye Rashid Kassian Mwaichande ameomba mamlaka husika kupunguza gharama ya kiapo kutoka Sh10,000 hadi Sh5,000, akieleza kuwa kiwango hicho ni kikubwa kwa baadhi ya wananchi.
Akijibu hilo, Diwani wa Kata ya Kivule, Rashid Manyinya amesema amesikia kilio cha wananchi na kufanya mazungumzo na wanasheria waliohusika, ambapo wamekubaliana kupunguza gharama ya kiapo hadi Sh5,000.
“Nawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi. Kama kuna changamoto au swali, waje waulize wataalamu waliopo ili wapate maelekezo sahihi na kupata vitambulisho vya NIDA,” amesema Manyinya.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kivule, Mohamed Salum, amesema zoezi hilo linawalenga zaidi wananchi wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea ambao hawana vitambulisho vya Taifa.
" Baadhi ya vigezo vinavyohitajika ni pamoja na cheti cha kuzaliwa, kitambulisho cha Taifa cha mzazi, au cheti cha kumaliza elimu ya msingi au sekondari, " na kusisitiza " wananchi wasio na nyaraka hizi watapata maelekezo kabla ya kuondoka eneo la zoezi hilo
Aidha, amesema zoezi hilo linahusisha pia wananchi kutoka kata jirani za Kipunguni, Kitunda, Majohe, Msongola na Mzinga.






Comments
Post a Comment