EID EL-FITRI 2026 KITAIFA KUFANYIKA DAR ES SALAAM RAIS SAMIA KUWA MGENI RASMI
Na Mwandishi wetu
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limetangaza kuwa maadhimisho ya Sikukuu ya Eid El-Fitri ya Kitaifa kwa mwaka 2026 yatafanyika katika Mkoa wa Dar es Salaam huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa Machi 12, 2026 na Katibu Mkuu wa BAKWATA Alhaj Nuhu Jabiri Mruma, sikukuu ya Eid El-Fitri mwaka huu inatarajiwa kuadhimishwa tarehe 20 au 21 Machi 2026, kutegemea kuandama kwa mwezi.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Swala ya Eid itaswaliwa katika Msikiti wa Mfalme Mohamed VI, Makao Makuu ya BAKWATA Kinondoni, kuanzia saa 1:30 asubuhi.
Baada ya swala hilo, Baraza la Eid la Kitaifa litafanyika katika Ukumbi wa Julius Nyerere Convention Centre (JNICC) kuanzia saa 9:00 mchana, ambapo viongozi mbalimbali wa serikali, dini na wananchi wanatarajiwa kuhudhuria.
BAKWATA imesema lengo la baraza hilo ni kuwakutanisha Waislamu na wananchi kwa ujumla katika kusherehekea kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani pamoja na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
Katika ujumbe wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Dkt. Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally Mbwana amewatakia Waislamu wote kumaliza vyema kumi la mwisho la mwezi mtukufu wa Ramadhani na kujiandaa na sikukuu ya Eid El-Fitri.
BAKWATA pia imewataka Waislamu na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika baraza hilo la kitaifa.

Comments
Post a Comment