SERIKALI YAONYA WAFICHA MAFUTA, YASISITIZA HAKUNA UHABA

 



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia mafuta na gesi asilia, Dkt. James Mataragio, ameonya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya watu watakaobainika kuficha mafuta kwa lengo la kuyauza kwa bei ya juu baadaye.

Pia amewataka wauzaji wa mafuta kununua bidhaa hiyo kwa kuzingatia mahitaji yao ya kawaida badala ya kuzidisha kiwango, akisema kufanya hivyo kunachochea hali ya uhaba usiokuwepo.

Dkt. Mataragio alitoa onyo hilo jijini Dar es Salaam mapema leo Machi 25,2026, alipofanya ziara katika Kampuni ya mafuta ya Cameil Oil, akisisitiza kuwa vitendo vya kuficha mafuta ni kinyume cha sheria na vinahujumu uchumi wa nchi.

“Tutakuwa wakali sana na kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kufanya hivyo kwani ni kinyume cha sheria na ni hujumu uchumi,” amesema 

Amewahakikishia wasambazaji wa mafuta pamoja na wananchi kwa ujumla kuwa hakuna upungufu wa mafuta nchini, akieleza kuwa hofu miongoni mwa baadhi ya wadau ndiyo inayochangia ongezeko la ununuzi usio wa kawaida.





Amesema mafuta yaliyopo yanatosha kukidhi mahitaji ya nchi, hivyo hakuna sababu ya wananchi au wasambazaji kukimbilia kununua mafuta kwa wingi au kuyahifadhi bila sababu.


Dkt. Mataragio amesema hofu ya uwepo wa uhaba imepelekea baadhi ya watu kubadilisha utaratibu wao wa kawaida wa matumizi, ambapo badala ya kujaza nusu tanki kama ilivyozoeleka, sasa wengi wanajaza hadi kujaa, jambo linalosababisha taharuki isiyo ya lazima.


“Hatuna upungufu wa mafuta, lakini watu wanaponunua zaidi ya mahitaji yao kwa hofu, wanasababisha hali ionekane kama kuna uhaba,” amesisitiza 

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa upatikanaji wa mafuta nchini na kuchukua hatua za mapema kuhakikisha upatikanaji wake unaendelea kuwa wa uhakika.





Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania  (EWURA), Dkt James Andilile amesema changamoto za upatikanaji wa mafuta duniani zimechangiwa na hali ya vita katika baadhi ya maeneo ya Mashariki, akibainisha kuwa Tanzania inaagiza mafuta kutoka Mashariki ya Kati.

Amesema kuwa hali hiyo imeongeza gharama za uagizaji mafuta, zikiwemo za usafirishaji, bima na ukodishaji wa meli, jambo linaloweza kuathiri upangaji wa bei za mafuta hapa nchini.




Hata hivyo, amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kufanya tathmini na vikao mbalimbali ili kuhakikisha bei ya mafuta inabaki kuwa himilivu na isiyoathiri uchumi wa nchi.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuondoa hofu na kuendelea kutumia mafuta kwa mahitaji yao ya kawaida, akisisitiza kuwa hakuna uhaba wa mafuta kwa sasa nchini.

Naye Katibu Mkuu wa wauzaji wa mafuta rejareja Tanzania,(TAPSOA), Tino Mmasi amesema wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na Serikali tangu kuanza kwa vita katika baadhi ya maeneo ya dunia kwa kufanya vikao mbalimbali ili kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea kuwa wa uhakika.

Aliwataka wafanyabiashara wa mafuta rejareja nchini kuendelea kuuza mafuta kwa utaratibu wa kawaida kwa kuwa bidhaa hiyo ipo ya kutosha kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.





“Nimedhibitisha mafuta yapo, nawahakikishia wananchi kuwa wasiwe na hofu wala wasiwasi kwamba bei zitapanda mwezi ujao,” amesema 

Ameongeza kuwa Serikali ni sikivu na tayari imeona changamoto hiyo, hivyo hakuna sababu ya kununua mafuta kwa wingi kwa lengo la kuyahifadhi kutokana na hofu ya kupanda kwa gharama za usafiri.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mafuta ya Cameil oil, Saleh Bajber amesema  kampuni hiyo imejipanga vizuri kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea kuwa wa uhakika kwa kipindi cha miezi miwili hadi mitatu ijayo.

"Kwa  mwezi Aprili, kampuni yetu imeagiza lita milioni 70 za mafuta kwa ajili ya kuhifadhi katika depo yao binafsi"amesema 




Ameongeza kuwa hadi sasa Camel Oil tayari imesambaza zaidi ya lita milioni 44 za mafuta, hatua inayolenga kuhakikisha huduma inaendelea bila usumbufu.

Comments

Popular posts from this blog

WANAFUNZI WALIOMALIZA KIDIA SEKONDARI WACHANGIA UJENZI WA KANISA SH MILLION 20

VETA YAJIPANGA KUSHIRIKINA NA TOYOTA TANZANIA KUIMARISHA MAFUNZO YA UFUNDI MAGARI

UJENZI WA BWAWA LA KUFUA UMEME LA MTO MALAGARASI , WAPIGA HATUA MPYA