BODI ZA WADHAMINI ZATAKIWA KUWAJIBIKA ZAIDI
Na Mwandishi Wetu,
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera, ametaka wajumbe wa bodi za wadhamini nchini, kuzingatia sheria, uwajibikaji na uadilifu katika kusimamia mali za taasisi wanazoongoza.
Amesisitiza kuwa hatua hiyo ni msingi muhimu wa kuimarisha utawala bora na kuchochea maendeleo endelevu ya jamii.
Akifungua mkutano wa wajumbe wa bodi za wadhamini ulioandaliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ukikutanisha washiriki wa mikoa ya Ruvuma, Njombe, Mtwara na Lindi mjini hapa juzi, alisema bodi hizo zina jukumu kubwa la kusimamia na kulinda rasilimali kwa manufaa ya wanachama na jamii kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa nafasi ya udhamini si heshima pekee, bali ni dhamana nzito inayohitaji uwajibikaji wa hali ya juu.
“Ni wajibu wa kila mdhamini kuhakikisha mali za taasisi zinalindwa na kutumika kwa malengo kusudiwa, si kwa maslahi binafsi,” alisema.
Alibainisha kuwa licha ya uwepo wa sheria, kanuni na miongozo, baadhi ya bodi zinakabiliwa na changamoto za ubadhirifu wa mali, migogoro ya uongozi na kushindwa kuzingatia katiba zao.
Alionya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria, dhidi ya watakaokiuka misingi ya utawala bora.
Katika kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi, Waziri aliiagiza RITA kuongeza kasi ya maboresho ya mfumo wa kidijitali wa eRITA, ili uwe rafiki zaidi kwa watumiaji na kuanzisha huduma za mkoba, zitakazofikia wadau maeneo ya pembezoni.
Waziri Homera pia alipongeza mafanikio ya RITA katika utoaji vyeti vya kuzaliwa na vifo ndani ya saa 48 kupitia eRITA, ambapo takwimu zinaonesha asilimia 94 ya maombi yanakamilishwa ndani ya muda huo.
Mafanikio hayo yalielezwa kuwa ni hatua kubwa katika kuboresha utoaji huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa taasisi.
Kabidhi Wasii Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi, alisema mkutano huo, wenye kaulimbiu ya ‘Uwajibikaji wa Bodi za Wadhamini kwa Ulinzi wa Mali za Taasisi na Maendeleo ya Jamii’, ni sehemu ya mkakati wa Wakala kuwajengea uwezo wajumbe wa bodi ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo.
Alisisitiza kuwa bodi zinapaswa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Bodi za Wadhamini Sura ya 318, ili kuhakikisha usimamizi bora wa mali na rasilimali za taasisi wanazosimamia.
Kanyusi alisema hadi Aprili mwakla huu, bodi 5,314 zimesajiliwa nchini, huku Ruvuma, Njombe, Mtwara na Lindi ikiwa na bodi 321.
Hata hivyo, alikiri kuwapo changamoto kadhaa, za welewa mdogo wa sheria, usimamizi usioridhisha wa mali na migogoro ya kiuongozi.
“Changamoto hizi ndizo zilizotusukuma kuanzisha programu ya mafunzo kwa wadhamini nchini, ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kanuni,” alisema.
Aliongeza kuwa RITA inaendelea kuboresha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kufanyia marekebisho sheria husika, ili kuimarisha usimamizi wa bodi.
Mkutano huo ni sehemu ya chachu ya kuimarisha usimamizi wa bodi za wadhamini nchini, huku ukisisitiza misingi ya uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika taasisi za umma na binafsi.



Comments
Post a Comment