CCM: UCHUMI WA CHAMA NI NGUVU YA SIASA

 



Na Mwandishi wetu, GEITA

CHAMA Cha Mapinduzi Kimesema siasa haiwezekani bila kuwa na uchumi imara, kwani nguvu na mafanikio ya chama chochote cha siasa inatokana na uimara wa uchumi wake na ndiyo msingi wa mafanikio ya chama hicho.

Katibu wa NEC Itikadi Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenan Kihongosi ameeleza hayo leo Aprili 17,2026 alipotembelea mradi wa kitega uchumi wa chama unaojengwa katika eneo la Sabasaba Kata ya Kalangalala Geita Mjini ikiwa ni muendelezo wa ziara yake mkoani Geita.

Kijongosi amesema,katika Mkutano Mkuu wa CCM uliopita walikuwa na maazimio 18 na miongoni mwa maazimio hayo kulikuwa na jukumu la kuimarisha uchumi wa chama pamoja na jumuiya zake na Geita imetekeleza maazimio hayo kwa vitendo.




“Wapo wanaouliza CCM inawezaje kufanya shughuli zake kwa ufanisi mkubwa, jibu ni rahisi sana tunajenga uchumi wa chama, tunawekeza, tunapata mapato, na mapato hayo yanawezesha shughuli zote za chama kuendeshwa kwa ufanisi,” amesema Kihongosi.

Ameongeza; “Ni ukweli usiopingika siasa bila uchumi haiwezekani na CCM kimeendelea kuwa kinara katika kuhakikisha kinaimarisha uchumi wake, huku kikisimamia pia maendeleo ya wananchi kupitia serikali yake”.

Amesema mradi huo  mkubwa unagharimu zaidi ya Sh bilioni tatu, ukiwa na zaidi ya vyumba vya biashara 212 na baadhi vimeanza kutoa huduma huku nyingine mikataba yake ikiwa imekamilika.

Amesema kwa maana hiyo muda si mrefu mapato yataanza kuingia kwenye akaunti za chama, chini ya usimamizi wa Baraza la Wadhamini akitoa wito kwa wanachama wa mkoa huo kuendelea kujitolea kujenga chama chao.

“Chama hiki kinajengwa na wanachama wenyewe, waasisi wetu walifanya kazi kubwa ya kutafuta maeneo, kuyamiliki na kuyaendeleza, leo sisi tunafaidi matunda yao.Hivyo basi, na sisi katika nafasi zetu tuendelee kununua maeneo mapya, kuyakatia hati, na kuendeleza miradi ili vizazi vijavyo vikute chama imara kiuchumi,” amesisitiza Kihongosi.

Ameongeza kwa kusisitiza kuwa eneo hilo la biashara si tu kwa ajili ya CCM pekee bali ni kwa wananchi na vyama vyote wanaruhusiwa kupanga na hata wasio na vyama pia wanaruhusiwa kwani CCM haina ubaguzi, bali inajli maslahi ya taifa kwanza.

Comments

Popular posts from this blog

WANAFUNZI WALIOMALIZA KIDIA SEKONDARI WACHANGIA UJENZI WA KANISA SH MILLION 20

VETA YAJIPANGA KUSHIRIKINA NA TOYOTA TANZANIA KUIMARISHA MAFUNZO YA UFUNDI MAGARI

UJENZI WA BWAWA LA KUFUA UMEME LA MTO MALAGARASI , WAPIGA HATUA MPYA