SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA MIFUMO YA AFYA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI






Na Hassan Kimweri, WAF - Dar es Salaam 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya afya duniani katika kukabiliana na changamoto zinazochangiwa na mabadiliko ya tabianchi, mabadiliko ya vipaumbele vya kimataifa, pamoja na maendeleo ya kisiasa na kiuchumi (geopolitics). 

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema hayo leo Aprili 16, 2026 alipokuwa anafungua Mkutano wa pili wa kimataifa wa shirikisho la jumuiya ya madaktari  wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.   

"Serikali ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha sekta ya afya inakuwa endelevu na imara, tunahitaji nchi yetu kuimarisha ukusanyaji wa rasilimali za ndani pamoja na kutumia mbinu bunifu za ufadhili wa huduma za afya," amesema Rais Samia 




Aidha, Rais Samia amefafanua kuwa Tanzania imejipanga kuendelea kuimarisha huduma za afya kwa wote kupitia utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote (Universal Health Coverage), sambamba na kuwekeza katika sekta ya tiba za kibingwa na bobezi, ikiwemo neurosurgery.

"Lakini pia, tnaendelea kuongeza uwekezaji katika maendeleo ya rasilimali watu kupitia mafunzo maalum, ufadhili wa masomo (scholarships), pamoja na ushirikiano wa kimataifa ili kuongeza idadi ya wataalamu wa upasuaji wa mishipa ya fahamu na taaluma nyingine za kibingwa," amesema Rais Samia 

Pia, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu na teknolojia ya afya kwa kujenga na kuimarisha hospitali za rufaa zenye vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa mfumo wa fahamu, pamoja na kupanua huduma za tiba kwa njia ya mtandao (telemedicine). 

Amesema, vifaa vya telemedicine tayari vimeshasambazwa katika hospitali zote za rufaa za ngazi ya juu na za mikoa, hatua inayosaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za kitaalamu kwa wagonjwa walioko maeneo pembezoni hususani vijijini .




Katika hotuba yake, Rais Samia pia ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba kupitia Bohari ya Dawa (MSD) ili kupunguza gharama na kuongeza ufanisi. 

Akihitimisha hotuba yake,Rais Samia amesema, Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wa kimataifa katika kuimarisha huduma za neurosurgery na mifumo ya afya barani Afrika na duniani kwa ujumla, kabla ya kutangaza rasmi kufungua Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Neurosurgery wa World Federation of Neurosurgical Societies.

Comments

Popular posts from this blog

WANAFUNZI WALIOMALIZA KIDIA SEKONDARI WACHANGIA UJENZI WA KANISA SH MILLION 20

VETA YAJIPANGA KUSHIRIKINA NA TOYOTA TANZANIA KUIMARISHA MAFUNZO YA UFUNDI MAGARI

UJENZI WA BWAWA LA KUFUA UMEME LA MTO MALAGARASI , WAPIGA HATUA MPYA