ACT Wazalendo YATANGAZA BARAZA KIVULI JIPYA
Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha ACT Wazalendo kimetangaza rasmi Baraza Kivuli jipya la Mawaziri kwa kipindi kinachofuata baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kikisema hatua hiyo inalenga kuimarisha usimamizi wa Serikali na kuendelea kuwa sauti mbadala ya wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari Mei 18, 2026, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu alisema matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 yameendelea kutoa uwakilishi mwembamba wa upinzani Bungeni, hali inayoongeza umuhimu wa vyama vya siasa kutumia mifumo mbadala ya kuisimamia Serikali, kuikosoa na kuibana ili iwajibike kwa wananchi.
Alisema chama hicho kitaendelea kutekeleza wajibu wake kama chama kinachoamini katika siasa za masuala kwa kuimarisha Baraza Kivuli lililoanzishwa rasmi kupitia Azimio la Halmashauri Kuu ya Taifa mwaka 2022.
Semu alisema azimio hilo lilimpa Kiongozi wa Chama mamlaka ya kuunda Baraza Kivuli kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata sauti mbadala yenye hoja na kuisimamia Serikali nje ya mhimili wa Bunge.
Aidha, alisema hili ni Baraza Kivuli la tatu tangu kupitishwa kwa azimio hilo mwaka 2022, akibainisha kuwa kwa kipindi cha miaka minne iliyopita chombo hicho kimekuwa nguzo muhimu katika kuibua changamoto za wananchi, kusukuma mijadala ya kitaifa kuhusu masuala ya msingi na kushawishi hatua mbalimbali za kisera na kiutendaji kutoka Serikalini.
Alieleza kuwa Baraza Kivuli hilo litakuwa tofauti na yaliyopita kwa kuwa mbali na kuwatumia wanachama wenye uwezo, uzoefu na weledi waliopo nje ya Bunge, pia litawahusisha wabunge waliopo Bungeni ili kupanua wigo wa usimamizi wa Serikali na kuimarisha ubora wa utendaji.
“Lengo letu ni kuhakikisha ACT Wazalendo inaendelea kuwa sauti imara ya wananchi ndani na nje ya vyombo rasmi vya dola,” alisema Semu.
Pamoja na hayo, alisema Baraza Kivuli hilo litasimamia uwajibikaji ndani ya Serikali na taasisi zake, akisisitiza kuwa taifa haliwezi kujengwa juu ya misingi ya kutowajibika, matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa rasilimali za umma bila kuwepo sauti thabiti ya kuhoji na kusimamia maslahi ya wananchi.

Comments
Post a Comment