CHALAMILA AITAKA WMA KUKOMESHA VIPIMO BATILI KULINDA HAKI ZA WALAJI






Na Mwandishi wetu

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameitaka Wakala wa Vipimo (WMA) kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara na kuchukua hatua stahiki za kisheria ili kutokomeza vipimo batili na kulinda haki za walaji.

Akizungumza kwenye soko la Kariakoo kuelekea Siku ya Vipimo Duniani, Chalamila amesisitiza umuhimu wa WMA kushirikiana kwa karibu na wafanyabiashara pamoja na mamlaka zingine kama TRA, TBS, na Tume ya Ushindani (FCC) ili kusimamia vyema sera ya vipimo vya mizani na uuzaji wa bidhaa mbalimbali.

Aidha, Chalamila amewatahadharisha wafanyabiashara kuwa tabia ya kupunguza vipimo ni dhambi kubwa na dhuluma inayomchukiza Mwenyezi Mungu na kukemewa na vitabu vyote vya dini, akihimiza utendaji wa haki katika biashara zao.




Sanjari na hayo, amewataka wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla kuendelea kudumisha amani ya nchi, kufanya kazi kwa juhudi, na kulipa kodi stahiki ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha huduma muhimu za kijamii.

Kwa upande wao, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo na mwakilishi wa WMA Francis Owelo wamebainisha kuwa vipimo sahihi ndio msingi wa usawa na haki katika shughuli za kila siku za biashara.




Siku ya Vipimo Duniani huadhimishwa kila ifikapo Mei 20 ya kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu maadhimisho hayo kitaifa yanatarajiwa kufanyika mkoani Dodoma chini ya kaulimbiu isemayo "Sayansi ya vipimo kujenga imani katika uundaji wa sera."

Comments

Popular posts from this blog

WANAFUNZI WALIOMALIZA KIDIA SEKONDARI WACHANGIA UJENZI WA KANISA SH MILLION 20

VETA YAJIPANGA KUSHIRIKINA NA TOYOTA TANZANIA KUIMARISHA MAFUNZO YA UFUNDI MAGARI

UJENZI WA BWAWA LA KUFUA UMEME LA MTO MALAGARASI , WAPIGA HATUA MPYA