MAWAKILI WA SERIKALI SIMAMIENI MASHAURI NA KUITETEA SERIKALI

 





Na Mwandishi wetu

MAWAKILI  wa Serikali wamehimizwa na kusisitizwa kuendelea kusimamia mashauri ya Serikali na kuitetea Serikali kwa ujumla katika vyombo vya ndani na nje ya nchi.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Katimba  wakati akifunga mafunzo kwa Mawakili wa Serikali wa kutoka Wizara mbalimbali, taasisi za Serikali, Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa wa Tanzania Bara na Zanzibar. Mafunzo hayo yameandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo yamefanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 18 hadi 22 Mei, 2026 jijini Arusha.

 Katimba amesema kuwa Serikali inawategemea sana Mawakili wa Serikali katika kulinda rasilimali za Taifa kupitia ushauri wa kisheria wenye tija na usimamizi madhubuti wa mashauri mbalimbali.



“Hivyo, baada ya mafunzo haya tunatarajia muweze kusimamia kwa ufanisi mashauri ya Serikali; kuimarisha usimamizi wa mikataba na manunuzi ya umma; kushauri vizuri Serikali kuhusu sheria za kodi, anga na uwekezaji; kusimamia kwa weledi usuluhishi wa migogoro; na kuitetea Serikali kwa ufanisi katika vyombo vya ndani na kimataifa,” amesema  Katimba.

Pia, ameongeza kuwa mafunzo hayo yamekuja wakati muhimu ambapo Taifa linaelekea katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi wa kati unaojumuisha wananchi wote. Ili kufikia malengo hayo, ni muhimu kuwa na taasisi imara za kisheria pamoja na wataalamu wenye uwezo wa kusimamia sheria, mikataba, uwekezaji, kodi na utatuzi wa migogoro kwa haki, uwazi na uwajibikaji.

“Kupitia ujuzi mlioupata, nina imani kuwa mtakuwa sehemu muhimu katika kuhakikisha kuwa sheria na mifumo ya Serikali inasimamiwa kwa weledi na kwamba matunda ya maendeleo yanawanufaisha wananchi wote kupitia mazingira bora ya uwekezaji, biashara na utoaji wa huduma za umma,” amesisitiza Katimba.

Comments

Popular posts from this blog

WANAFUNZI WALIOMALIZA KIDIA SEKONDARI WACHANGIA UJENZI WA KANISA SH MILLION 20

VETA YAJIPANGA KUSHIRIKINA NA TOYOTA TANZANIA KUIMARISHA MAFUNZO YA UFUNDI MAGARI

UJENZI WA BWAWA LA KUFUA UMEME LA MTO MALAGARASI , WAPIGA HATUA MPYA