SERIKALI YAKAGUA MRADI WA MABASI YA UBIA DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
KITUO cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kimefanya ziara ya kukagua mradi wa mabasi unaomilikiwa na Kampuni ya Mofat, unaotekelezwa kwa ushirikiano na Mamlaka ya Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) jijini Dar es Salaam.
Akizugumza mara baada ya kufanya ukaguzi Katika eneo la mbagala Mkurungezi wa Kituo cha Ubia, David Kafulila amesema ukaguzi huo umefanyika kwa kuzingatia matakwa ya kisheria yanayohitaji miradi ya ubia inayohusisha Serikali kufuatiliwa kwa karibu kuanzia hatua za maandalizi hadi mwisho wa utekelezaji wake.
Alisema Lengo kuu la ziara hiyo lilikuwa ni kutathmini uendelevu wa uwekezaji huo, ambao unatajwa kuwa muhimu katika kuboresha huduma za usafiri ndani ya jiji la Dar es Salaam.
Alisema Katika ukaguzi huo, changamoto kadhaa zimebainika, ikiwemo kuwepo kwa mabasi 50 yaliyopo katika mradi huo ambayo hayatumiki tangu yaliponunuliwa kutokana na kukosa nafasi ya kuendesha huduma katika baadhi ya maeneo.
Aidha, imeelezwa kuwa licha ya kampuni kutumia mabasi 50 kwa sasa, mabasi mengine mapya yamekaa bila kutumika kwa zaidi ya nusu mwaka.
Amesema jukumu lao ni kuhakikisha miradi ya aina hiyo inakuwa endelevu na inaleta tija kwa wananchi pamoja na Serikali.
Kwa upande wake, msemaji wa Kampuni ya Mofat, Philip Changala amesema mradi huo ni wa kimkakati kwa ajili ya manufaa ya wananchi, hususan katika maeneo wanayoyahudumia kuanzia Mbagala hadi Kivukoni, pamoja na Gerezani na Boma.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya mradi huo yanategemea ushirikiano mzuri kati ya Serikali na sekta binafsi, akibainisha kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji binafsi kushiriki katika miradi ya maendeleo.
“Tumeweza kubuni huduma zinazolenga makundi mbalimbali ya wananchi ili kuhakikisha watu wengi zaidi wanapata huduma hii,” amesema.
Aidha, amewataka wananchi kuacha kutumia miundombinu ya barabara za mwendokasi kinyume na utaratibu, akieleza kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha changamoto katika uendeshaji wa huduma.
Hata hivyo, amesema mradi huo bado upo katika hatua za awali, hivyo baadhi ya changamoto zinazoendelea kujitokeza zinatarajiwa kupatiwa ufumbuzi kadri utekelezaji unavyoendelea.



Comments
Post a Comment