MD TWANGE -UKOPESHAJI MAJIKO UMEME UMEFANIKIWA KWA ASILIMIA 90
Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Lazaro Twange amesema amemweleza Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi hatua zinazochukuliwa na shirika hilo katika kutekeleza mkakati wa nishati safi ya kupikia, ikiwemo utekelezaji wa mpango wa kukopesha majiko ya umeme kwa wananchi kupitia mfumo wa Bill Financing.
Twange amesema hayo wakati akizungumzia mambo muhimu aliyomueleza Rais Wa Zanzibar, Dkt Hussein Ali Mwinyi alipotembeleza banda hilo lililopo katika maonesho ya 50 ya biashara ya kimataifa maarufu kama Sabasaba.
Amesema mpango huo unawawezesha wateja wapya pamoja na waliopo kupata majiko ya umeme kwa mkopo na kulipa taratibu kupitia ununuzi wa umeme.
"Kwa sasa tuna mpango unaoitwa Bill Financing ambao unaendelea. Wateja wetu wapya na wale ambao tayari wanatumia umeme wanaweza kukopeshwa majiko na wakawa wanalipa mkopo wao kadri wanavyonunua umeme," amesema.
Amesema mpango huo umepata mwitikio mkubwa na kufikia mafanikio ya zaidi ya asilimia 90, hali iliyochochea TANESCO kushirikiana na sekta binafsi katika kuupanua.
Ameeleza kuwa tayari mikataba imesainiwa na wadau hao na kazi ya kukopesha majiko ya umeme kwa wananchi imeanza rasmi.
Pia ametoa wito kwa wananchi kutumia umeme kama nishati ya kupikia, akisema tayari watumiaji waliopo wameonesha kuwa ni nishati yenye gharama nafuu zaidi ikilinganishwa na nishati nyingine.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo amesema pia amemweleza Rais Dkt. Mwinyi kuhusu maendeleo ya mradi mkubwa wa kujenga njia mpya za kusafirisha umeme kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar.
Amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa njia tatu za kusafirisha umeme chini ya bahari, zitakazotoka Dar es Salaam kwenda Unguja, Tanga kwenda Pemba pamoja na Tanzania Bara kwenda Mafia.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uwezo wa kusafirisha umeme mwingi zaidi kwenda Zanzibar, hatua itakayokidhi ongezeko la mahitaji ya umeme kufuatia maendeleo makubwa ya ujenzi yaliyoshuhudiwa visiwani humo.


Comments
Post a Comment